Header Ads

Header ADS

Mhe. Pauline Gekul amewaagiza Maafisa Utamaduni Nchini kusimamia Vyema Mfuko wa Utamaduni na Sanaa

 Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amewaagiza maafisa utamaduni nchini kusimamia vyema Mfuko wa Utamaduni na Sanaa katika ngazi za mikoa na halmashauri ili kuhakikisha wasanii walioko katika maeneo yao wanapata mikopo kupitia mfuko huo.

 Mhe.Gekul ametoa maelekezo hayo Januari 26, 2023 jijini Dodoma alipofungua Kikao Kazi cha Baraza la Sanaa la Taifa na Maafisa Utamaduni nchini, ambapo amewataka maafisa hao kutekeleza vyema majukumu yao ya kuendeleza utamaduni na sanaa nchini.

 "Kila mmoja atambue shughuli za utamaduni na sanaa zinazofanyika katika eneo lake, toeni elimu kuhusu Mfuko wa Utamaduni na Sanaa namna wasanii wanavyoweza kukopa, kurejesha pamoja na taratibu nyingine," amesisitiza Mhe. Gekul.

 Pamoja na hilo, Naibu Waziri Gekul amewasisitiza maafisa hao kusimamia maadili ya Taifa pamoja na kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii, huku akiwasisitiza kutoa elimu shuleni kuhusu umuhimu wa Wimbo wa Taifa pamoja na kuhakikisha wimbo huo unaimbwa kwa usahihi.

 Aidha, amewataka maafisa hao kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kufuata taratibu na miongozo ya namna ya kukusanya maduhuli hayo.

 Awali, akimkaribisha Naibu Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Ndd. Saidi Yakubu amesema kikao hicho kimehudhuriwa na M

maafisa 119, ambacho pamoja na mambo mengine kitasaidia kuboresha utendaji wa maafisa hao baada ya kupata Semina ya miongozo mipya, kanuni na taratibu mbalimbali ambazo zimehuishwa kwa maslahi ya sekta hizo.

 Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Dkt. Kedmnon Mapana amesema kikao hicho cha siku mbili kinatarajia kutoa maazimio yenye lengo la kutatua changamoto ya upotevu wa mapato pamoja na usimamiaji wa utamaduni na sanaa katika ngazi ya mkoa na halmashauri.






 

No comments

Powered by Blogger.