Waandishi 6 wakamatwa kutokana na kuvuja kwa video inayomuonyesha rais akitokwa na haja ndogo hadharani
Waandishi sita wa habari nchini Sudan Kusini wamekamatwa kutokana na kusambaa kwa picha za video zinazomuonyesha Rais Salva Kiir akitokwa na haja ndogo, mashirika ya kutetea haki za vyombo vya habari yanasema.
Mnamo Desemba, video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionekana ikimuonyesha Bw Kiir akijikojolea huku wimbo wa taifa ukipigwa kwenye hafla.
Wafanyakazi sita kutoka shirika la utangazaji la serikali walikamatwa wiki hii. Kamati ya Kulinda Wanahabari (CPJ) sasa inataka waachiliwe.
Patrick Oyet, rais wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Sudan Kusini, aliambia Reuters kwamba waandishi hao "wanashukiwa kufahamu video hiyo ilivujaje".
Shirika la Utangazaji la Sudan Kusini (SSBC) linasema video hiyo hiyo haikuonyeshwa kwenye kituo hicho.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini Michael Makuei aliiambia Sauti ya Amerika kwamba watu wanapaswa kusubiri kujua kwa nini wanahabari hao walikamatwa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu mara kwa mara yametaka mamlaka za Sudan Kusini kuacha kuwanyanyasa na kuwatishia waandishi wa habari.
Bw Kiir alikua rais wa kwanza wa Sudan Kusini - nchi mpya zaidi barani Afrika - mnamo 2011. Lakini nchi hiyo imekumbwa na mizozo mingi tangu wakati huo, ikivumilia migogoro ya kikatili, machafuko ya kisiasa, majanga ya asili na njaa.
No comments
Post a Comment