Washitakiwa nane akiwemo Mwanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania [JWTZ]
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasomea masharti ya dhamana washtakiwa nane akiwemo mwanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanaodaiwa kukutwa na nyara za serikali ambazo ni Kobe 116 bila ya kuwa na kibali.
Hata hivyo, washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, wamesomewa masharti ya dhamana bila ya wao kuwepo mahakamani kutokana na changamoto za usafiri kutoka gerezani
Akisoma masharti hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Rhoda Ngimilanga amewataka washtakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoishi Dar es Salaam, wenye barua na vitambulisho vya Nida na watakaosaini bondi ya sh. Milioni tano.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni, mfanyabiashara Josephat Moyo (52) mkazi wa Tabata, Deogratius Lugeng'a (40), MT 88046 Sajenti Cosmas Ndomba kutoka JWTZ na Mfanyabiashara Hamza Abdalah ( (52)
Wengine ni MT 118102 Kassim Abdalah (35), Nkanamuli Ngaza (52) mlinzi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na wakukima wawili Kutoka mkoa wa Dodoma ambao ni Stephano Chedego (51) na Mwaluko Mgomole.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu Uchumi yenye mashitaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na nyara za serikali ambazo ni kobe 116 bila kibali.
Inadaiwa, kati ya Januari mwaka hadi Julai 3 mwaka 2022 ,Dar es Salaam, washtakiwa hao waliendesha genge la uhalifu kwa kununua, kukusanya, kusafirisha, kununua na kuuza nyara za serikali ambazo ni Kobe 116 wenye thamani ya USD 8120 sawa na sh 18,935,840.
Katika shitaka la pili imedaiwa, katika tarehe isiyojulikana mkoani Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na nyara hizo za serikali kwa kununua na kuziuza bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia, Julai 3 mwaka 2022 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, washitakiwa hao walikutwa na kobe hao bila kuwa na kibali
Kesi hiyo imeahirishwa hado Januari 30, 2023 washtakiwa watakapoletwa mahakamani kwa ajali ya kuangalia kama upelelezi umekamilika na kudhaminiwa iwapo watakuwa wametimiza masharti ya dhamana.
No comments
Post a Comment