Header Ads

Header ADS

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuja na majibu kamili

 

   Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuhakikisha tarehe ijayo wanakuja na majibu kamili juu ya upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande na wenzake.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Ramadhani Rugemalila amesema hayo leo Februari 7, 2023 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kuelezewa kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Rugemalila amesema, kwa kuwa washtakiwa wako nje kwa dhamana basi kesi hiyo inaarishwa lakini amewataka upande wa mashtaka kuhakikisha wanakuja na taarifa kamili juu ya upelelezi dhidi ya kesi hiyo.

Amesema sheria inasema mashauri kama haya yanapaswa kufikishwa mahakamani upelelezi ukiwa umekamilika kabla shauri halijafunguliwa.

Mapema wakili wa serikali Kaima Mosie alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi katika shauri hilo bado unaendelea na kwamba jalada la kesi bado liko Dodoma kwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini likiwa bado linafanyiwa kazi kwa ajili ya maamuzi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 2,2023 itakapokuja kwa ajali ya kutajwa.

Mbali na Kipande washitakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Mashaka Kisanta , Ofisa Rasilimali Watu, Peter Gawile, Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi, Casmily Lujegi na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Kilian Chale.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8 (sawa na Sh bilioni 4.2).

Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, mwaka 2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam, walikula njama na kuisababishia TPA hasara.

Pia, wanadaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 17 mwaka 2015, wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .

Inadaiwa kati ya Oktoba Mosi mwaka 2014 na Oktoba Mosi mwaka 2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP).

No comments

Powered by Blogger.