Header Ads

Header ADS

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii awataka asikari wa Uhifadhi sheria na miongozo wanapotakeleza majukumu yao

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Askari wa Uhifadhi katika maeneo mbalimbali nchini wazingatie sheria kanuni,taratibu na miongozo pindi wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo kulinda Maliasili.

Ameyasema hayo leo Wilayani Ushetu Mkoani Shinyanga mara baada ya kutembelea Kata ya Mlowa wakati wa ziara yake kikazi yenye lengo la kutatua changamoto baina ya wananchi na wahifadhi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka wananchi wake waishi kwa amani bila taharuki ya aina yoyote, hivyo Askari wa Uhifadhi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria.

“Sisi tumepewa dhamana ya kusimamia maliasili kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, katika kutekeleza jukumu hili hatupaswi kuleta taharuki kwa wananchi” amesisitiza Mhe. Mary Masanja.

Amewaeleza wananchi hao kuwa mtu yeyote anapovunja sheria kwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa bila vibali lazima utaratibu wa kisheria ufuatwe ikiwemo kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi hao waendelee kufuata sheria na kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia, amewataka Askari Uhifadhi waandae programu za kutoa elimu kwa wananchi ili wajue umuhimu na faida za uhifadhi ikiwemo kuleta mvua, kutunza vyanzo vya maji,kuchavusha mazao na kusaidia katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

Naye,Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita amesema ataendelea kushirikiana na wahifadhi kuhakikisha elimu ya uhifadhi inaendela kutolewa kwa wananchi wanaozunguka Pori hilo.

No comments

Powered by Blogger.