Nape kufungua kongamano la 12 la kitaaluma
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari anatarajiwa kufungua Kongamano la 12 la Kitaaluma la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), linalotarajiwa kuanza tarehe 29 Machi 2023, mjini Morogoro.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kongamanbo hilo la siku nne, Neville Meena ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF amesema, pamoja na Nape, pia jukwaa hilo linategemea kuwepo mgeni mwingine ambaye ni Dk. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria.
“Kongamano hili huwa tunafanya kila mwaka kwenye mikoa mbalimbali, safari hii tumeamua kufanyia hapa Morogoro,” amesema.
Kwenye kongamano hilo, Meena amesema kutakuwa na mada sita ambazo ni Utendaji wa Vyombo vya Habari, Taaluma na Maadili; Wanawake katika habari na hatari ya kutoweka kwao kwenye vyumba vya habari.
Mada zingine ni Uchumi wa Vyombo vya Habari na jinsi ya kuvinusuru; Mabadiliko ya Teknolojia, Ukuaji na Ujenzi wa Mitandao ya Kijamii yenye viwango vya kitaaluma; Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria za Habari na mweleko wake.
Amesema, mada ya mwisho itakuwa Vyombo vya Habari na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Uchaguzi sio tukio, ni mchakato. Inahitajika kuandaa watu na kuwashawishi kushiriki kwenye uchaguzi, vyombo vya habari vinawekeza fedha kwenye uchaguzi huo, hivyo ni sehemu muhimu kwenye kongamano hili,” amesema.
Jane Mihanji, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF amesema, miongoni mwa sababu kuweka mada inayohusu wanawake na vyombo vya habari ni kutokana na tafiti kuonesha kwamba, kuna unyanyasaji wa wanawake kwenye vyombo vya habari.
“Tumekuwa tukihimiza kuwa na ushiriki sawa. Baadhi ya tafiti zinaonesha wanawake wanaopewa nafasi za juu ni wachache.
Tafiti za TAMWA, Internews na zingine zinaonesha kuwa, kumekuwa na unyanyasaji wa wanawake kwenye vyumba vya habari.
“Taarifa zao zimekuwa hazitoki hivyo, wamekuwa wakikimbia vyumba vya habari,” amesema Jane.
No comments
Post a Comment