Serikali ya Zambia yaonya uhamasishaji wa haki za watu wa mapenzi ya Jinsia moja
Serikali ya Zambia imeonya kuwa haitavumilia uhamasishaji wa wa haki za watu wa mapenzi ya jinsia moja ikisema kuwa ni kinyume na maadili ya Kikristo nchini humo.
Onyo hilo limetolewa siku moja baada ya polisi kuwakamata wanaharakati wanne kutoka kundi la wanaharakati wa kike kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kuhusu maandamano yaliyopangwa. Kundi hilo lilifanya maandamano yaliyoidhinishwa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia Jumapili kabla ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, lakini maafisa walisema ilikuwa mbinu ya kuhamasisha ushoga.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa Jack Mwiimbu aliiambia VOA Jumatano kwamba serikali yake haihamasishi haki za wapenzi wa jinsia moja na msimamo wake imeuelezea tangu serikali ilipoingia mamlakani karibu miaka miwili iliyopita.
Alilaani maandamano yaliyoandaliwa na Taasisi ya Sistah Sistah, akisema ni kinyume na maadili na sheria za Zambia.
"Napenda kuwatahadharisha wananchi kutoruhusu na kukiuka sheria kwa makusudi kwa kutumia mazingira yaliyopo yanayoruhusu uhuru wa kujieleza na kukusanyika" alisema mwiimbu.
Naye Naibu Msemaji wa Polisi wa Zambia Dan Mwale aliiambia VOA waandamanaji hawakufuata kanuni za vibali, ambazo ziliwaruhusu tu kupinga haki za kingono na kijinsia na kutohamasisha haki za wapenzi wa jinsia moja.
"Uchunguzi umeongezeka, wakati huo huo polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu programu na shughuli za Taasisi ya Sistah Sistah" alisema Mwale.
Taasisi ya Sistah Sistah ilikataa kutoa maoni yake lakini ilitoa taarifa kwenye mtandao wa Twitter ikisema inashangazwa kwamba maandamano hayo ambayo inasema yalilenga kuangazia unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake, yamegeuzwa kuwa mawimbi ya kutisha ya chuki katika mijadala ya hadhara, haswa mitandaoni.
Kundi hilo lilisema washukiwa hao wanne waliachiliwa kwa dhamana ya polisi Jumatano na hivi karibuni watafikishwa mahakamani.
Washukiwa watatu wameshtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo kwa afisa wa umma na, ikiwa watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa jela miaka saba.
Mwanzilishi mwenza wa kundi hilo Mwangala Monde pia ameshtakiwa kwa mkusanyiko usio halali, na iwapo atapatikana na hatia anaweza kukabiliwa na kifungo cha ziada cha miezi sita jela.
Taarifa hiyo iliongeza kusema kuwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana umekuwa wa kawaida, na kusababisha watu wengi kutouzingatia.
Ripoti za hivi karibuni za polisi zinaonyesha kuwa zaidi ya kesi 20,000 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2022 pekee, nyingi zikiwahusisha wanawake na wasichana.
Maandamano ya wikiendi, yaliyohudhuriwa na takriban watu 300, yamezua mjadala nchini Zambia, huku watu wengi wakishutumu maandamano ya Sistah Sistah kwa kutangaza haki za wapenzi wa jinsia moja na kutaka shirika hilo kupigwa marufuku.
Wengine walisema wakati umefika kwa Wazambia kuruhusiwa kujadili masuala kama hayo ili waweze kuamua njia ya kusonga mbele.
Katika taarifa baada ya maandamano msemaji mkuu wa serikali Chushi Kasanda pia alilaani tukio hilo, ambalo anasema lililenga kutangaza haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Zambia.
Ngono ya watu wa jinsia moja hairuhusiwi chini ya ya adhabu ya nchi, ambayo inaharamisha vitendo kinyume na maadili dhid ya utaratibu wa asili na uchafu mbaya sana.
Sheria hiyo, ambayo ilianza tangu wakati wa ukoloni wa Uingereza, ina adhabu ya kifungo cha miaka kumi na nne jela.
No comments
Post a Comment