Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji amesema kuwa chama chao hakitaweza kupoteza mvuto kwa upande wa Zanzibar licha ya aliyekuwa Katibu Mkuu CUF, Maalim Seif Sharif ambaye anatajwa kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi visiwani humo. kutangaza kuhamia ACT – Wazalendo.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na kituo kimoja cha redio, ambapo Dkt. Mashinji amesema wananchi wa Zanzibar bado wanakikumbuka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Siasa ni mtazamo, kama wamefanikiwa kuwaaminisha wananchi kuwa itakuwa hivyo basi wamefanikiwa, lakini siasa wakati wote inabadilika wananchi wa Zanzibar waliipigia CHADEMA 2015, nina imani wananchi bado hawajasahau kuwa CHADEMA ni kipenzi chao.
Aidha, kuhusiana na ACT kujiunga UKAWA, Mashinji amesema kuwa kwa mazingira ya kisiasa kwasasa wanahitaji kuungana pamoja ili kuhakikisha wanapambana zaidi na chama tawala CCM ili waweze kuking’oa madarakani.
Hata hivyo, siku za hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt Vincent Mashinji alimpongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif kwa hatua yake ya kujiunga na Chama cha ACT- Wazalendo na kusema uamuzi wake ni sahihi.