Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewahimiza vijana kuwa wazalendo na kuithamini nchi yao.
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuwaaga vijana waliopanda Mlima Kilimanjaro Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Amesema kuwa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alikuwa kiongozi mzalendo kwa nchi yake na alijali utu na usawa, hivyo ni vyema vijana na vizazi vijavyo wakarithishwa falsafa za Baba wa Taifa.
“Vijana mna kila sababu kuyaenzi matendo ya Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere na Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume kwa vitendo kwa kuwa ninyi ndio nguzo ya Taifa na mnaelewa vyema tulipotoka, tulipo na tunapoenda,” amesema Mhagama
Aidha, amesema kuwa Viongozi hao hawakuwa wabinafsi kwa kujilimbikizia mali na hawakubagua mtu kwa rangi wala kabila bali walijenga Taifa na kudumisha amani na moja.
Mhagama ametoa rai kwa vijana kuwa wazalendo na kuwasihi wafanye kazi kwa bidii ili kujenga Taifa kupitia uchumi wa viwanda utakao ifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
             Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba amesema kuwa tukio hilo ni muhimu kwa vijana kutambua historia na mchango wa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere katika Taifa.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, James Kajugusi amesema kuwa Baba wa Taifa alianza harakati za kulikomboa Taifa akiwa kijana na aliendelea kufanya hivyo kwa kuwahamasisha vijana kujenga Taifa lao baada ya kupata uhuru.