Header Ads

Header ADS

Mh.Stella Ikupa Auasa Uongozi wa Muheza kushirikisha walemavu katika masuala ya ukimwi

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri mkuu,Mh Stella Ikupa anayeshughulikia masuala ya walemavu ameuasa Uongozi wa halmashauri ya wilaya ya muheza kuhakikisha unatoa elimu na huduma ya masuala ya UKIMWI kwa jamii nzima.
   Hayo ameyasema wakati akizungumza na Watendaji wa Halmashauri hiyo mkoani tanga wakati wa ziara yake ya siku tatu alipokuwa akikagua shughuli zinazofanywa wilayani hapo zinazohusu masuala ya UKIMWI.
   
 












Pia amedai kuwa kwa kipindi kirefu kundi la walemavu limeachwa nyuma sana hususani katika kujumuishwa katika masuala ya elimu na mahitaji ya kijamii hivyo ni muhimu kuzingatia mahitaji yao na kuendelea kuwapa elimu ili waweze kunufaika na kupunguza maambukizi katika mkoa huo wa Tanga.
“Ni vyema kuhusisha kundi la wenye ulemavu katika upatikanaji wa huduma za masuala ya Ukimwi kwa kuzingatia kundi hili limekuwa likisahaurika na kutofikiwa kama yalivyo makundi mengine,”alieleza Mhe.Ikupa
   Aidha ameongeza kuwa mikakati iliyowekwa na halmashauri hivi sasa ni kuhakikisha kunakuwepo na mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma za masuala ya UKIMWI,Utoaji elimu juu ya mabadiliko ya tabia na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU,kuwashirikisha katika program mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya kuimarisha mifumo ya utoaji elimu ya watu wanaishi na VVU na namna pia ya kusaidia makundi hayo.
   Mh.Mwanashaa Rajab ambaye ni Mkuu wa wilaya ya muheza amesema kuwa bado wanaendelea kuwafikia watu wenye ulemavu katika huduma za upimaji,utoaji wa huduma za dawa na kuendelea kuwashirikisha walemavu katika masuala yanayohusuUKIMWI ili kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na Tisini Tatu
 “Tunakushukuru kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zetu na kukuahidi tutatekeleza maagizo yako ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti zinazojumuisha mahitaji maalum ya wenye ulemavu, kuwapatia elimu, kuwafikia na kuendelea kuwashirikisha katika program mbalimbali za kimaendeleo,”alisema Mwanashaa.
  Pia Mratibu wa kuthibiti masuala ya UKIMWI katika wilaya hiyo Herieth Nyangasa alieleza kuwa hali ya maambukizi katika kipindi cha mwaka 2018 ni asilimia 2.1 kutoka 2.6 asilimia kwa mwaka 2017 ambapo imepelekewa na juhudi za Serikali za kufikisha elimu kwa walemavu.
   “Zipo jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha wanapunguza hali ya maambukizi mapya na kuwapatia huduma watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na wilaya kuwa na vituo 445 vya kutolea huduma ya ushauri nasihi na upimaji wa VVU, vituo 20 vya upimaji kwa hiari, vituo 38 upimaji kwa ushawishi na vituo 45 vya huduma ya kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,”Alesema Nyangasa
  Naye Dkt Yahaya Mbura ambaye ni Mratibu wa kuthibiti Ukimwi wilayani humo alieleza changamoto zinazokwamisha jitihada za Serikali katika kuwahudumia watu wanaoishi na VVU kuwa ni pamoja na utoro wa watumiaji wa dawa zinazofubaza Virusi vya Ukimwi.
  “Hadi sasa tuna ripoti za utoro kwa wanaotumia dawa wapatao 388 na hii imechangiwa na changamto za miundombinu kipindi cha mvua, umbali wa vituo kutoka katika makazi yao pamoja na uwepo wa imani potofu kuhusu matumizi ya dawa hizo,”alisisitiza Dkt. Yahaya.

   

No comments

Powered by Blogger.