Takriban Abiria 74 Wafariki Baada Ya Treni Waliyokuwa Wakisafiria Kuwaka Moto Pakistan
Takriban abiria 74 walifariki wakati treni iliokuwa ikisafiri kutoka mji wa Karachi Pakistan kuelekea Rawalpindi iliposhika moto.
Waziri wa reli, Sheikh Ahmed, alisema kwamba moto huo ulisababishwa na kulipuka kwa mtungi wa gesi uliokuwa ukitumiwa na abiria kupikia kiamsha kinywa mwendo wa asubuhi.
Moto huo unadaiwa kusambaa hadi katika mabehewa matatu, kulingana na maafisa walionukuliwa katika vyombo vya habari vya eneo hilo.
Abiria wanaoingia na stove katika treni ili kupika chakula wakati wa safari ndefu ni swala la kawaida waziri huyo aliongezea.
Aliongezea kwamba abiria wengi walikuwa wakielekea katika kongamano lililoandaliwa na vuguvu la dhehebu la Kisuni Tablighi Jamaat.
Ajali hiyo ilitokea karibu na Rahim Yar Khan kusini mwa mkoa wa Punjab. Treni hiyo iliokuwa ikisafiri kutoka Karachi kupitia maeneo mengi ya Pakistan hadi Rawalpindi inaitwa Tezgam mojawapo ya treni za zamani ambayo ni maarufu sana.
Inahudumu kila siku na inachukua saa 25 na nusu.
Pakistan ina historia ya ajali za gari moshi zinazosababisha maafa mengi. Waathiriwa huwa wengi kwa kuwa treni hizo hubeba watu wengi zaidi ya viwango vyao.
Tarehe 11 mwezi Julai , watu walifariki katika ajali , huku wengine wanne wakifariki katika ajali nyengine mwezi Septemba.
Mwaka 2007, takriban watu 56 waliuawa na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa katika ajali karibu na eneo la Mehrabpur.
Mwaka 2005, zaidi ya watu 130 waliuawa wakati treni tatu zilipogongana katika mkoa wa Sindh katika kile kilichotajwa kuwa ajali mbaya zaidi inayohusisha treni kuwahi kutokea.
No comments
Post a Comment