Header Ads

Header ADS

Bunge la Tanzania limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria itakayomwezesha mtu kujipima mwenyewe virusi vya ukimwi

Bunge la Tanzania limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria itakayomwezesha mtu kujipima mwenyewe virusi vya ukimwi na pia kushusha umri wa vijana kuweza kupima virusi vya ukimwi bila ya ridhaa ya mzazi, hadi kufikia miaka 15.
Naibu Waziri wa Afya Dokta Faustine Ndugulile amesema Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekubali na kuridhia malengo ya dunia yanayojulikana kama 90-90-90, ikimaanisha kwamba asilimia 90 ya Watanzania wanaoishi na virisi vya ukimwi kuweza kupimwa na kutambua hali yao ya maambukizi.
kifaa cha kujipimia Ukimwi
Asilimia 90 ya wale waliopimwa waweze kufikiwa na kupata dawa, asilimia 90 ya wale watakaopata dawa kuweza kufubaza virusi vya ukimwi.
Hata hivyo amesema yote hayo kuweza kufanikiwa kikamilifu inategemea na asilimia 90 ya kwanza ya watu kupima na kujitambua afya zao.Naibu Waziri wa Afya ameeleza kuwa mabadiliko hayo ya sheria kuhusu ukimwi yamekuja pia kutokana na changamoto zilizopo za upimaji wa virusi vya ugonjwa huo.
''... Changamoto imekuwa wanaume wengi hawajitokezi kupima kwa sababu ya uoga na vitu vingine, lakini takwimu pia zinaonesha kuwa maambukizi mengi mapya kwa sasa ni kwa vijana.
Asilimia 40 ya maambukizi mapya ni vijana, ambako katika hiyo asilimia 40, 80 ni wasichana''.
Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania anasema kutokana na changamoto hizo, ndio maana serikali ikaona umuhimu wa kuja na njia mpya, ikiwemo kuruhusu mtu kuweza kujipima mwenyewe.
Hata hivyo, amesema ili mtu kuanza kutumia dawa atahitaji kujithibitisha tena kwa kwenda kupima katika kituo cha afya.
 Awali upimaji wa virusi vya ukimwi ulikuwa lazima ufanyike vituo vya afya na mpimaji lazima awe muhudumu wa afya.
Aidha Dokta Ndugulile amesema kwa kuanzia kutakuwa na maeneo maalumu ambayo watu wataweza kununua vipimo hivyo, huku wauzaji wakiwa wamepata utaalamu na elimu ya kutosha na kwamba mnunuzi atapewa pia elimu na ushauri nasaha na utaratibu unaofuata baada ya kupima.
Aidha amesema lengo la baadaye ni kuweka katika maduka ya dawa na kuuzwa kama vipimo vingine kama vile cha kupima ujauzito.
Hata hivyo ipimaji binafsi hautaruhusiwa kwa vijana wa umri wa miaka 15, kutokana na kwamba vijana hao wataruhusiwa tu kupima katika vituo vya afya, hivyo hawatauziwa vipimo hivyo.
'' Kikubwa tutaendelea kutoa elimu, na kwamba Tanzania sio nchi ya kwanza kufanya hivyi, nchi nyingine za Afrika mashariki wameshapitisha sheria hii, Kenya, Uganda pamoja na nchi nyingine za SADC
Ameongeza kusema kuwa kwa kuona maambukizi yamekuwa makubwa kwa vijana.
Hata hivyo, Muswada huu wa mabadiliko ya sheria juu ya Ukimwi, ambao tayari umepitishwa na bunge utaanza kufanya kazi baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kutia saini ya kuuridhia.
Ukimwi
Hata hivyo, mabadiliko haya yanaonekana kupokelewa na hisia tofauti tofauti , Ibrahim Joseph mkazi wa Dodoma yeye anaona kuwa mabadiliko haya ya upimaji wa vvu yanaweza kuwa na madhara kwa sababu hakuna ushauri nasaha, "Itakuwa mtu anajipimia tu nyumbani kwake, akiamua kujidhuru inakuwa ni rahisi kwa sababu anaona kwamba ameathirika".
"Kwa jina naitwa Hamida Ramadhan, mimi naona kuwa ina manufaa na taarifa unakuwa nayo wewe mwenyewe."
Kwa upande mwingine baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa mabadiliko haya yanaweza kuifanya serikali kushindwa kupata takwimu za uhakika wa watu walioathirika 
Majaribio tayari yamefanyika kuhusiana na vipimo hivi vya ukimwi.
Takriban watu milioni moja na laki nne wanaishi na virusi vya ukimwi kwa sasa nchini Tanzania, ambapo watu milioni moja na laki moja wameweza kufikiwa na kupatiwa matibabu.

No comments

Powered by Blogger.