Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu, Shinyanga Limeagiza kuwachukulia sheria baadhi ya wakandarasi wa umeme wa REA.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga limeagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme (REA) ambao wanawatoza wananchi fedha ili kulipia gharama za nguzo na mita kinyume na maagizo ya serikali.
Wakizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Tabu katoto diwani wa kata ya Igunda na Paulo Sai Golani diwani wa kata ya Kisuke wamesema wananchi wamekuwa wakitozwa fedha na baadhi ya watumishi wa kampuni ya ANGELIQUE INTERNATIONAL.CO.L.T.D ambayo inatekeleza Mradi wa REA katika vijiji 54 katika halmashauri hiyo.
“Mimi katika kata ya Kisuke wananchi wangu wametozwa zaidi ya shilingi laki moja kwaajili ya kulipia gharama za nguzo huku wengine wakilipia shilingi elfu 10 kwaajili ya Mita na wakikaidi kulipa hawapatiwi huduma hii ya umeme wa REA”, Golani ameeleza.
"Katika Kata yangu ya Igunda huduma ya umeme imetolewa kwa urasimu kama huna fedha huduma hii inakuruka na inapelekwa katika nyumba za matajiri pekee na kwa wananchi maskini imekuwa ni ngumu huku maeneo muhimu kama visima, shule na zahanati yakirukwa”,alisema Katoto.
Pia, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu Juma Kimisha alisema kitendo hicho kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwani si maadili ya kazi yao na maelekezo ya serikali wananchi wengi wameshindwa kupata huduma hiyo kutokana na urasimu uliopo katika miradi ya REA.
Naye,Afisa Masoko wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutoka Makao makuu Musa Chowo akijibu malalamiko hayo, alimtaka meneja wa TANESCO wilaya ya Kahama Mhandisi King Fokanya kuhakikisha anawasimamia vizuri wakandarasi ambao hadi sasa wamebainika kuwepo na tabia ya kuwaibia wananchi wa halmashauri hizo.
“Nimetoa mawasiliano yangu kwenu mikiwaona wakandarasi wanaowaibia wananchi toeni taarifa kwa vyombo vya usalama na wakamateni kwani hao ni sawa na wezi wengine na wanatekeleza hayo kwa matakwa yao binafsi na sio maelekezo ya serikali”,alisema Chowo.
Kampuni ya ANGELIQUE INTERNATIONAL CO LTD inayotekeleza mradi huo mpaka sasa imeweka umeme katika vijiji 14 kati ya 54 vya halmashauri ya Ushetu kandarasi ambayo imedumu kwa miaka miwili ambayo kwa sasa muda wake umeshamalizika na hajakamilisha mradi huo.
No comments
Post a Comment