Upande Wa utetezi wa Kesi Ya Kutekwa Kwa Mo Dewji umeulalamikia upande wa Jamhuri kuchelewesha upelelezi wa kesi hiyo.
Upande wa utetezi katika kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu Mo, umeulalamikia upande wa Jamhuri kuchelewesha upelelezi na kwamba mshtakiwa anateseka mahabusu.
Mshtakiwa, dereva wa teksi Mousa Twaleb, anakabiliwa na kesi ya kumteka mfanyabiashara huyo pamoja na wenzake wanne ambao bado hawajakamatwa na kufikishwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.
Wakili wa utetezi, Maufudhu Mbagwa, alidai kuwa Septemba 16, mwaka huu, upande wa Jamhuri uliomba hati za kukamatwa kwa watuhumiwa wengine ambao hawajakamatwa.
Pia,alisema kama inawezekana upande wa Jamhuri unaweza kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo kwa upande wake, ufanye hivyo kuliko kuleta hati ya mashtaka ya watu wengi ambao hawajulikani watakamatwa lini.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Glory Mwenda, alidai kuwa anaomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Aidha,Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa Novemba 25, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.
Pia,Watuhumiwa wengine ambao hadi sasa hawajafanikiwa kuwakamata na upande wa mashtaka unaendelea kuwatafuta ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara huyo.
Washtakiwa hao ambao hawajakamatwa ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.
No comments
Post a Comment