Maandamano dhidi ya mauaji ya maafisa wa Ebola huko Ituri yafanyika DRC
Shambulio hilo katika vituo viwili vya matibabu lililofanyika katika eneo la Ituri linadaiwa kutekelezwa na waasi wa Maimai ambao ni wapiganaji kutoka eneo hilo.
Wanaharakati hao pia wamekasirishwa na mauaji ya wanakijiji 19 katika kijiji cha Maleki, mjini Beni karibu na mpaka na Uganda.
Shambulio hilo linadaiwa kutekelezwa na waasi wa ADF.
Wanasema serikali na Umoja wa mataifa wamewaacha raia chini ya usimamizi wa washambuliaji hao.
Kiongozi wa kitengo cha dharura dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC Jean Kacques Muyembe ametaja mashambulio ya vituo hivyo viwili na mauaji hayo ya wahudumu watatu kuwa pigo kuu.
Bwana Jean amesema kwamba atafanya mazungumzo na vyombo vya habari muda wowote kuanzia sasa ili kuelezea kuhusu hali ilivyo.
Mapema siku ya Alhamisi waasi hao walivishambulia vituo viwili vya matibabu vya Ebola vinavyoendeshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), katika uvamizi uliofanyika usiku wa kuamkia Alhamisi na kuwauwa wahudumu watatu.
Taarifa zinasema kuwa miongoni mwa watu waliouawa ni wafanyakazi wa WHO na kwamba watu wengine wanne wamejeruhiwa vibaya.
Kwa mujibu wa mashuhuda, waasi waliwazidi nguvu polisi kwenye vituo hivyo vilivyopo katika maeneo yaMangina na machimbo ya Biakato.
Magari manne yamechomwa moto pamoja na majengo kadhaa yameteketezwa.
Kupitia ujumbe wake wa Twitter, maafisa wakuu wa shirika hilo akiwemo Mkurugenzi Mkuu Bwana Tedros Adhanom Ghebreyesus wamelaani shambulio hilo lililosababisha vifo na majeruhi:
Hii si mara ya kwanza kwa mashambulio ya aina hii kutokea katika vituo vya Ebola nchini humo.
Mashambulio ya wanamgambo na ukosefu wa imani ya jamii kwa wafanyakazi wa afya mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamekuwa ni kikwazo cha juhudi za kudhibiti mlipuko wa hivi wa Ebola ambao ni hatari kwa taifa hilo na mataifa mengine jirani.
Makundi ya waasi yenye silaha yamekuwa yakishambulia mara kwa mara vituo vya tiba ya Ebola, huku kukiwa kuna ukosefu wa imani miongoni mwa jamii za wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa na Ebola ambao wanalaumu wageni kwa mlipuko wa maradhi hayo.
Hali hiyo inachangia juhudi za kukabiliana na mlipuko huo kuwa ngumu katika majimbo yenye mizozo ya Ituri na Kivu.
Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilisema kuwa watu 300,000 wamesambaratika kufuatia ghasia katika eneo hilo katikakipindi cha mwezi huu pekee.
No comments
Post a Comment