RAIS MAGUFULI AAGIZA MAJENGO YOTE YA OFISI ZA TANROAD DUMILA YAWE KITUO CHA AFYA.
Rais Magufuli ameagiza majengo yote yaliyokuwa ya Ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania(TANROAD) eneo la Dumila mkoani Morogoro yakabadilishwe na kuwa Kituo cha Afya Dumila.
Ametoa maagizo hayo leo Novemba 20,mwaka 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Dumila akiwa safari kuelekea mkoani Dodoma. Akiwa hapo wananchi hao kupitia diwani wao walitoa maombi yao kadhaa kwa Rais ambayo kwao yamekuwa changamoto ikiwemo ya kukosa kituo cha afya, uhaba wa maji safi na salama na umeme.
Hivyo wakati anajibu changamoto hizo, Rais amesema kuanzia leo hii, majengo hayo ya ofisi za TANROAD yatakuwa Kituo cha afya Dumila na nyumba 11 za ofisi hizo ziwe nyumba za watumishi wa kituo hicho.
"Hoja zote ambazo zimetolewa na diwani wenu hapa ni za msingi na zitafanyiwa kazi, hili la kituo cha afya, naagiza majengo ya ofisi ya Tanroad yawe kituo cha Afya, kuhusu madaktari, dawa na vifaa tiba hilo nitatoa maagizo kwa Wizara ya Afya.
"Kesho Diwani mje mfungue kituo cha afya na andika jina lako kwa niaba yangu, nimekuruhusu.Yale majengo yalijengwa kwa fedha za Serikali, kuna nyumba 11 nazo zote ziwe za kituo cha afya Dumila,"amesema Rais Magufuli.
Pia Rais amesema changamoto nyingine ambazo zimeelezwa na wananchi hao zitafanyiwa kazi huku akitumia nafasi hiyo kutoa ruhusa ya wananchi hao kuchimba mchanga katika daraja la Mto Dumila ingawa ametaka kuwepo na utaratibu mzuri ambao uchimbaji huo hautaharibu daraja hilo.
"Nawaruhusu mchimbe mchanga, lakini tukubaliane kwa utaratibu mzuri, tusiharibu hili daraja.Ikitoke mkachimba mchanga na kuharibu daraja matipa yote nitayakamata,"amesema Rais Magufuli.
No comments
Post a Comment