Header Ads

Header ADS

Watumishi wa afya katika Mkoa wa Dodoma wajikuta wakati mgumu.

     Mara baada ya kubainika kufanya kazi kinyume na taratibu zinavyo elekeza. Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Daktari Dorothy Gwajima amesema, kutokana na kukithiri kwa utendaji wa mazoea kwa baadhi ya watumishi wanaopima upepo sasa kaguzi zote zitaanza kufanyika kwa mwelekeo wa kutathmini jinsi gani kila mtumishi wa kada husika ametekeleza majukumu yake kama yalivyoelekezwa kwenye muundo wake wa utumishi.
   Ambapo, amewaeleza watumishi hao kuwa, inaonekana maboresho yanayoonekana katika kituo hicho yakawa yanafanywa na watumishi wachache wanaofidia utegaji wa wengi hivyo, kutokana na mwenendo huo sasa hatasita kuwashtaki wazembe wote kwa Katibu Mkuu utumishi ili hii habari ya kupandishana vyeo iende sambamba na chujio makini la ufanisi wa kila mtumishi na kiongozi mahala pa kazi.















    Aidha,hatua hiyo  imekuja kufuatia ufuatiliaji endelevu unaofanywa na Naibu Katibu Mkuu na jopo la wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kituo hicho na vingine nchini ambapo, kituo cha afya Makore ni mojawapo ya vituo vinavyojengewa uwezo viwe vya mfano katika mabadiliko ya mifumo ya uwajibikaji mahala pa kazi. Mwelekeo huu ni utekelezaji wa mojawapoa ya Azimio la Kikao cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika Agosti, 2019 kuwa, kila halmashauri iteue vituo 4 vya mfano.
       “Sitasita kumshauri Katibu Mkuu Utumishi asiridhie baadhi ya watumishi miongoni mwa 80 mnaowaombea wapandishwe vyeo iwapo nitabaini ufanisi wao hautoshi kupitia kaguzi tunazofanya. Nitamwambia Katibu Mkuu hawa watumishi hawastahili kupanda vyeo kwakuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na hapa msisingizie eti mko wachache wakati idadi yenu ni mara mbili ya wanaotakiwa hapa,” alisema Gwajima na kusisitiza kuwa,“haiwezekani zaidi ya miezi mitatu wataalamu wa kitengo cha dawa eti hawajahuisha taarifa za dawa kwenye kitabu husika (Ledger) yaani mnajifanyia fanyia tuu bila utaratibu halafu mnasema dawa hazitoshi huku mmeotesha vichaka vyenye utata wa kujua wapi mmezitumia?” alihoji Gwajima.
     Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu pia, alifanya uhakiki wa hadi ujazo wa kila kitendanishi cha maabara kwamba kilitakiwa kupima sampuli ngapi na mwisho kimepima ngapi ambapo, alibaini wataalamu wa maabara wamepima sampuli nyingi zaidi kuliko walizotakiwa kupima huku wakiwa hawana kumbukumbu za kiofisi kuhusu wapi walikopata vitendanishi vya ziada, ‘inakuwaje ulitakiwa kwa kitendanishi hiki upime sampuli 50 badala yake umepima 350”? Gwajima alihoji.
    Naye mtaalamu wa Maabara katika kituo hicho Ndugu Godfrey Mahundi hakuwa na majibu yakina juu ya wapi hasa alitoa ziada hiyo ya vitendanishi na kama ipo sehemu alikotoa kwa nini hakuna rekodi ya aliyempa wala yeye kukiri mapokezi.
     Lakini pia,Dkt. Gwajima alisema, kwa kawaida taratibu za uchukuaji dawa lazima ziwe zinaandikishwa kutoka eneo moja hadi lingine yaani kutoka hifadhi kuu, hifadhi ya kati, hifadhi ndogo mpaka zinapomfikia mgonjwa na hata kama amepewa toka kwenye kituo kingine lazima kuwe na rekodi za aliyetoa na aliyepokea.
    “Hapa Kituo cha Afya Makore baadhi ya watumishi wameelewa somo hasa eneo la huduma za kitabibu na kiuguzi ila nyie watu wa maabara na dawa ndiyo bado mnapima upepo mnajifanyia mambo kienyeji kwa kutoandika kumbukumbu za matumizi ya raslimali za dawa na vitendanishi na nani katumia, nasema nyie pamoja na wengine wote nchi nzima wanaofanya mambo kama yenu ambayo, yanayoruhusu kushamiri kwa vichaka vya matumizi mabaya ya raslimali za vituo sasa wakati umefika wa kuamua kurudi kwenye mstari ama mtausikia tu utumishi wa umma kwenye redio. Aliendelea kusisitiza Katibu Mkuu.
     Amesema kituo hicho ni cha mfano na watakaofanya hapa lazima wawe wa mfano na si vinginevyo, huwezi kuwa mtumishi wa kituo cha mfano huku wakitoa fursa ya majizi kujificha kwenye kazi zao. Ameongeza kuwa ijulikane kuwa hizo ni salamu zake kwa vituo vyote vya afya nchini.
    Katika hatua nyingine Watumishi hao walionesha kutambua uzembe walioufanya na kukiri kuzembea katika utendaji wao huku wakiomba msamaha na kuahidi kubadilika.















     Akikiri kufanya uzembe Mfamasia wa Jiji la Dodoma George Hondi, kwa niaba ya watumishi wengine, alisema wanaona fedheha na aibu kwani yote yaliyobainishwa na Naibu Katibu Mkuu hakuna hata moja la kusingiziwa wala kuonewa.
    “Ni kweli hatujatekeleza na kusimamia majukumu yetu na hili ni kosa na sisi tuseme tu na kunaahidi kubadilika” alisema Hondi.
   Kwa mujibu wa Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Namba 1 wa Mwaka 2009 unaoeleza juu ya Miundo ya Utumishi kwa Kada za Afya chini ya Wizara ya Afya yapo mambo mengi ambayo yameendelea kugundulika kupitia ziara hii na zingine za Naibu Katibu Mkuu na timu yake na yanayotokana na baadhi ya watumishi kujifanyia kazi kienyeji mfano, Mfamasia Daraja la Pili anayo majukumu yake ikiwemo kutunza kumbukumbu za dawa na vifaa tiba na kutekeleza maelekezo ya wizara kuhusu ufanisi wa Kamati ya Dawa kwenye kituo husika lakini wengi hawafanyi na sababu hawana lakini wanadai wapandishwe vyeo Hii haiwezekani” amesema Dkt Gwajima. .
     Chini ya OR-TAMISEMI imeundwa timu rasmi ya kuwa inafanya ukaguzi wa utekelezaji wa majukumu ya kila mmoja tutajua huko huko wapi hawatoshi na wapi wako idadi kubwa lakini hawana tija.
    Hata hivyo,Dkt. Gwajima amewataka Makatibu wa Afya kutokuwa makarani wa kuorodhesha tu majina ya watu kupanda vyeo kisa mtumishi kaajiriwa siku nyingi bali wapime ufanisi ili kumtendea haki anayejituma na mzembe naye apate haki yake ya kutopandishwa cheo au kushushwa. Amesema wataimarisha mifumo na taratibu za kujipima na kuwapima watumishi ili haki itendeke haraka kwa wale wanaojituma na wasiojituma pia wapate haki yao mapema tu kila mtu abebe mzigo wake.
     Lakini pia  juma lililopita, Naibu Katibu Mkuu akifungua Kikao cha Wafamasia wa Mikoa mjini Dodoma, aliwarushia lawama wataalam wa Afya hususani kada ya Famasia kwamba, wizi wa dawa unaoshamiri unachangiwa na usimamizi mbovu eneo lao kiasi kwamba dawa hizo zinapotea bila taarifa kwa kuwa hawazingatii au kwa makusudi wanafanya kazi huku wakitoa fursa nzuri kwa wezi na wadokozi kutekeleza azma yao na hii ni kusaliti juhudi za Serikali za kuongeza bajeti ya dawa na kufikia bilioni 269, hivyo akaapa kupambana nao kwa kuomba nguvu za wananchi kuwafichua wote watakaobainika kuhujumu jitihada hizo.


No comments

Powered by Blogger.