Dosari Uchaguzi Serikali Za Mitaa Zamuibua James Mbatia
Mbunge wa Vunjo James Mbatia amemtaka Waziri wa nchi tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) kuongeza muda wa zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu katika vituo vilivyoripotiwa kuwa na dosari mbalimbali kama walivyofanya wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura.
Mbatia ameyabainisha hayo katika kikao chake na waandishi wa Habari kuzungumzia mapungufu yaliyojitokeza mpaka sasa katika zoezi la uchukuaji fomu za kushiriki kugombea uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Amesema baadhi ya maeneo yameripotiwa kuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kufungwa kwa vituo na wasimamizi kutofahamu utaratibu hali ambayo imechangia kutopatikana kwa fomu hizo kwa wakati na kwamba kwa kuongeza muda itakuwa imefidia siku zilizopotea na kuheshimu rasilimali muda.
“Kuwa watu wamejitokeza kuchukua fomu lakini vituo vilikua vimefungwa mfano Moshi kuna maeneo hata leo vituo havina wasimamizi sasa kama wachukua fomu hawakuti wasimamizi wanakata tamaa maana muda ni siku saba zikipotea siku mbili si sawa namuomba Waziri mwenye dhamana aongeze siku ili kufidia,” amefafanua Mbatia.
Ameongeza kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa ni mkubwa na una maslahi mapana kwa Taifa na kwamba uwepo wa dosari kadhaa unakuwa ni ishara mbaya na tishio kwa usalama wa nchi kwani ulipaswa kuheshimiwa na kuangaliwa kwa jicho la pili katika ustawi wa maendeleo hasa kiuongozi.
Ameeleza kuwa waliopewa dhamana ya kusimamia taratibu za uchaguzi huu walipaswa kuzingatia au kuheshimu kanuni na miongozo na kwamba mkanganyiko unaotokea unaweza kusababisha migogoro inayoweza kuleta machafuko.“Migogoro inaondoa na kuvunja utu maana hakuna majawabu sahihi yanayotolewa na mara kadhaa nimesikia matamko ya TAMISEMI lakini hayatekelezwi wala kuchukuliwa hatua kama hakuna kuaminiana wadau wakutane ili kujadili jambo hili na hatua za haraka zichukuliwe kunusuru utata uliopo,” ameongeza Mbatia.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa kituo cha Demokrasia nchini (TCD) amesema kimsingi suala hilo si la kulinyamazia kwa maslahi na uhai wa taifa kwani kinachoonekana ni baadhi ya watu kushindwa kutenganisha kati ya viongozi na watendaji kitu kinachopelekea kuibuka kwa migogoro.
“Na tayari kuna malalamiko yanatoka ndani ya vyama hata CCM kinayoongoza Serikali nao wanalalamikia dosari hapo ndio ujue kuna hali isiyo shwari wapo pia CUF, ACT, NCCR, CHADEMA na vyama visivyo na wabunge yani hakuna kuaminiana suala hili si lankunyamaza,” amezidi kusisitiza Mbatia.
Hata hivyo Mbunge huyo wa Vunjo amesisitiza kuwa watendaji wanaosimamia zoezi hilo kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na mamlaka zilizo juu yao kutokana na wengi wao kutoelewa utaratibu kiasi cha kuleta mkanganyiko na kwamba waondoe maslahi binafsi.
“Tusiangalie maslahi binafsi ya chama au vikundi ili kulinda amani ya nchi yetu tunahitaji kuwa wamoja kwani wale wote wanaogombea waangalie upana wa uongozi wao badala ya kuwa na maono binafsi maana wasipo zingatia hayo ni hatari kwa Taifa,” amesisitiza Mbatia.
Oktoba 30, 2019 Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo alikiri uwepo wa dosari kadhaa katika zoezi la uchukuaji fomu na kudai kuwa tayari wameanza kuzifanyia kazi na kuwataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni ili kuepuka malalamiko yaliyoanza kutolewa.
Aidha,Alisema zipo kata 3959 nchini na kati ya kata hizo ni 72 pekee ambazo zilikuwa na dosari na kwamba zoezi hilo halikufanyika kiufasaha na kuyataja baadhi ya maeneo yenye malalamiko kuwa ni pamoja na Liwale Lindi, Moshi, Sengerema na Songwe.
Hata hivyo, Sambamba na hatua hiyo pia Jafo alivitaka vyama vyote vya siasa kuhakikisha vinafuata kanuni, sheria na masharti wakati wote wa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za ugombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuepusha uvunjifu wa sheria.
No comments
Post a Comment