Header Ads

Header ADS

Mbowe atoa onyo kali Uchaguzi wa CHADEMA

          Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekemea vitendo vya rushwa na kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii katika chaguzi za chama hicho.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo  katika mkutano wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha). Katika mkutano huo utafanyika uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo.

      Uchaguzi ndani ya chama hicho utahitimishwa Desemba 19, 2019 utakapofanyika uchaguzi wa katibu mkuu, naibu katibu wakuu Bara na Zanzibar pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu. Desemba 18, utafanyika uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar.

Tayari Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na baraza la wazee yamepata viongozi wake.

Katika uchaguzi wa Bawacha, Halima Mdee anagombea peke yake nafasi ya mwenyekiti. Wanaowania umakamu mwenyekiti Bara ni Hawa Mwaifunga, Aisha Luja, Marceline Stanslaus na Mary Nyagabona, kwa upande wa Zanzibar ni Mariam Salum Msabaha, Sharifa Suleiman na Zeud Mvano Abdulahi.

Katika hotuba yake leo Mbowe amesema, “nimesikia kuna harufu ya rushwa katika uchaguzi huu. Leo unatafuta uongozi ndani Chadema kwa rushwa? Hiki siyo chama nilichokijenga.”

"Fitina na kutukanana kwenye mitandao ya kijamii sio jambo zuri. Nakemea jambo hili na tutawachukulia hatua wote watakaobanika kufanya vitendo hivi, msivyokuwa waadilifu sasa mnachukua huku na kule halafu mnawaambia tupo pamoja," amesema Mbowe.

Amewataka wagombea kupambana na kwa hoja huku akitoa wito wa wajumbe wa mkutano huo kutowachagua viongozi kwa kigezo cha rushwa badala yake wasikilize na kuwapima kulingana na sera zao wakati wa kujinadi.

"Bawacha tunaiamini na inafanya kazi nzuri lakini ina mdomo. Mtu yeyote atakayejiingiza kwenye vitendo vya rushwa hakitakii mema chama hiki, shiriki uchaguzi kwa haki na upendo. Leo kampeni za kina mama zinafanywa na wanaume? Kuna maisha baada ya uchaguzi," amesema mwenyekiti huyo.

No comments

Powered by Blogger.