Afya, Elimu Kuendelea Kutolewa Bure Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa elimu bure kwa wananchi wake kama ilivyo kwa sekta ya afya na katu haitorudi nyuma.
Rais Dkt. Shein ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Skuli ya Sekondari Ziwakije Wingwi Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamrashamra za sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo Rais Dkt. Shein amesema kuwa elimu itaendelea kutolewa bure na kueleza kuwa yeyote ambaye atabadilisha malengo ya Serikali ya kutoa elimu na afya bure atachukuliwa hatua zinazofaa kwani hayo ni matunda ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Rais Dkt. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Mapinduzi na harakati zake za kupigania huru wa wanyonge na kusema kuwa Mapinduzi yamekuja kutokana na madhila makubwa yaliokuwa wakifanyiwa Waafrika wa Zanzibar.
No comments
Post a Comment