Mbunge wa Jimbo la Dodoma ameahidi kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali kwa jiji la Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde ameahidi kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali kwa jiji la Dodoma kwa kuvipatia mafunzo endelevu ya masuala ya Ujasiriamali na Biashara na kuhakikisha vinapata mikopo ya uhakika kuimarisha mitaji yao.
Mbunge Mavunde ameyasema hayo leo wakati akifunga Kongamano la Mafunzo ya Ujasiriamali lililojumuisha takribani wajasiriamali 1000 kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma ambapo Wajasiriamali hao wamepata nafasi ya kufundishwa kwa vitendo namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kupitia Taasisi ya chuo cha elimu kwa wote kwa ushirikiano na Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Jiji la Dodoma.
"Nitaendelea kuhakikisha nafadhili mafunzo haya kitarafa na kwenye kata kupeleka walimu na nyenzo za mafunzo kwa kila kata ili wananchi wengi zaidi wanufaike na hivyo kupelekea kuchangamkia fursa kubwa ya kiuchumi iliyopo Dodoma kwa sasa na baadaye kupitia vikundi vya Ujasiriamali tuweze kuvikopesha ili kuongeza mitaji yao. Jiji la Dodoma kwa sasa tuna fedha za kutosha kukopesha vikundi vya Wakina Mama, vijana na watu wenye ulemavu kwa kiwango cha juu kuliko ilivyokuwa awali hivyo nitoe rai kwa wananchi kutokaa nyuma katika hili" Alieleza Mavunde
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Shariffa Nabalang'anya amesema Idara yake imejipanga kusimamia mafunzo ya elimu ya ujasiriamali ili mikopo itakayotolewa ilete tija na manufaa kwa wananchi na kufikia malengo yanayotarajiwa.Akishukuru kwaniaba ya Wajasiriamali wenzake Bi. Sarah Sylivestre amemshukuru Mbunge Mavunde kwa ufadhili wa mafunzo hayo kwa kuwa yamewaongezea kitu kikubwa sana na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kama chanzo cha kujiingizia kipato.
Hata hivyo Kupitia shughuli zao na hivyo kujikwamua na umaskini wa kipato,na kumshukuru zaidi Mbunge kwa uwezeshwaji wa vifaranga 20,000 na mashine za viwanda vidogo vidogo zenye thamani ya Tshs 55,000,000
Aidha kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Chuo cha elimu kwa wote Bw. Saravai Izila ameahidi kushirikiana na Wajasiriamali hao hatua kwa hatua kwa ufuatiliaji ili kuhakikisha mafunzo waliyopatiwa yanaleta tija na kuchochea kukua kwa shughuli za kiuchumi za wajasiriamali hao.
No comments
Post a Comment