Sekta Ya Madini Kuchangia Asilimia 10 Ya Pato La Taifa Ifikapo 2025
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hatua iliyofikiwa ya kuzuia uvunaji haramu wa rasilimali kwa utaoji wa cheti cha uhalisia kwa madini ya bati, kutaiwezesha sekta ya madini nchini kuchangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Ameyasema hayo jana (Jumapili, Februari 23, 2020) wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Waziri Mkuu ambaye amezindua utoaji wa cheti cha uhalisia (certificate of origin) kwa madini ya bati kitakachokuwa kinatolewa na Tanzania, amesema cheti hicho ni muhimu kwa Taifa letu na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maziwa Makuu kwa kuwa kitaweka utaratibu wa kudhibiti madini hayo.
Waziri Mkuu amesema mambo waliyojifunza katika mkutano huo yatasaidia kuongeza kasi ya kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. “Wizara ya Madini shirikianeni na wadau wengine katika kuhakikisha mkutano huu unaendelea kuboreshwa kila mwaka na kuongeza washiriki ili kupanua uelewa wa pamoja.”
Waziri Mkuu amesema kuwa ni matarajio ya kila mmoja wao kwamba uzinduzi huo walioufanya utasaidia katika kutekeleza Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa Rasilimali yaani ‘Protocol Against the Illegal Exploitation of Natural Resources’
“…nafahamu kwamba mkutano wa aina hii unaoihusu sekta ya madini unafanyika kwa mara ya pili hapa nchini. Nitoe wito kwa nchi wananchama kuhakikisha mikutano ya aina hii iweze kuandaliwa katika nchi nyingine na iwe endelevu katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa zilizopo nchi nyingine.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inaridhishwa na kuimarika kwa utendaji kazi wa sekta ya madini nchini kutokana na mafanikio yake ikiwemo kuongezeka kwa mchango wake katika pato la Taifa. “Mathalan, kupitia Taarifa ya Hali ya uchumi ya Mwaka 2019, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020, mchango wa Sekta ya Madini ulikua kwa asilimia 13.7.”
Waziri Mkuu amesema kwenye kipindi hicho, sekta ya madini ilikuwa ya pili katika kuchangia pato la Taifa ikitanguliwa na sekta ya ujenzi ambayo ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 16.5.
“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya sh. bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya lengo la mwaka la kukusanya sh. bilioni 470.89.Makusanyo hayo yalitokana na mrabaha, ada ya ukaguzi wa madini, huduma za kimaabara, mauzo ya machapisho mbalimbali ya kijiolojia na ada za leseni.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi. “Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 kote nchini.”
Amesema masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake, hivyo ametumia fursa hiyo kuwafahamisha wadau wa mkutano huo kuwa masoko hayo yapo wazi kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa nchi ambazo bado hazijaanzisha masoko ya madini kutumia masoko yaliyoko nchini wakati wakijipanga kuanzisha masoko yao.
“Masoko haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa sambamba na kuanzishwa kwa masoko ya madini, Serikali pia imefanikiwa kuhamasisha wamiliki wa migodi kuchangia zaidi katika huduma za jamii nakuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo wa madini.
“Vilevile, Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali katika kumiliki na kusimamia migodi, ikiwa ni pamoja na kumilikishwa asilimia 16 ya hisa katika migodi;na kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi.”
Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano huo umehudhuriwa na nchi 11 wanachama waJumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) pamoja na wadau wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Biteko alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa madini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo wachimbaji, wanaotengeneza na kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande wa Serikali kujifunza namna ya kuboresha na kuifanya sekta ya madini kuwa ni sekta yenye kuongeza tija kwa Taifa.
No comments
Post a Comment