Watumishi Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Watakiwa Kutunza Siri
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima amewataka watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufanya kazi kwa kushirikiana, uwajibikaji na kutunza siri za ofisi kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi Tawi la NIDA, Kailima alisema mafanikio ya Mamlaka hiyo ni pamoja na kushirikiana katika utendaji wa kazi ili kuleta weledi, na pia kuepuka kutoa siri za ofisi kwa mujibu wa utaratibu wa utumishi wa umma.
Pia aliwakumbusha watumishi hao kutoka Makao Makuu ya NIDA na Ofisi zake Mikoani, kuhakikisha uwajibikaji unakuwepo kwa upande wa mwajiri na mwajiriwa kwa kufanyiwa kazi kile kinachotakiwa kufanyiwa kazi na kisichohitajika kuifanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
“Tukoseane kwa nia ya kuboresha, tusikoseane kwa nia ya kubomoa kwa sababu ya kupata fursa hii ya kuwa na haki na hadhi sawa, na pande zote mbili ziwajibike kuwajibishana,” alisema Kailima.
Aliongeza kuwa, watumishi wanapaswa kupewa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka na masuala yanayowahusu kwa utaratibu wa ofisi au unaoidhinishwa na Mkurugenzi Mkuu na si vinginevyo.
“Muhakikishe mnatoa huduma kwa wananchi sehemu zote nchini kwa weledi, maafisa wafike mapema katika maeneo ya kazi na kutoa vitambulisho vya Taifa mapema, na wananchi waridhike na huduma hiyo mnayoitoa, kwa hatua hiyo mtapunguza malalamiko ya wananchi,” alisema Kailima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Arnold Kihaule alitoa mafanikio ya Mamlaka yake hadi kufikia Desemba mwaka 2019, alisema NIDA imefanikiwa kusajili wananchi 21,511,321, Wageni wakaazi, 19,311 na Wakimbizi 274,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Pia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imezalisha namba za utambulisho 16,211,654 na kutoa vitambulisho 5,787,869, na vimewafikia wananchi ilipofika mwezi Desemba 2019,” alisema Dkt. Kihaule.
Kikao cha Baraza hilo cha siku moja pia kilipitia Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2019/20 kwa Kipindi cha kwanza cha Mwezi Julai hadi Desemba na Makadirio ya Bajeti ya Mamlaka kwa Mwaka wa Fedha 2020/21.
No comments
Post a Comment