Header Ads

Header ADS

TRA imewataka wafanyabiashara na wachuuzi kutojihusisha na biashara za Magendo.

     Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara na wachuuzi wanaoishi jirani na fukwe za Bahari ya Hindi kutojihusisha na biashara za magengo kwani kufanya hivyo ni kuisababishia nchi kukosa mapato yake stahiki kutokana na wahusika wa biashara hizo kukwepa kulipa kodi.
     Akizungumza na wafanyabiashara hao katika fukwe za bahari za Msasani, Mbweni, Ununio, Beach kidimbwi na Kunduchi zilizopo jijini Dar es Salaam, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi, Rose Mahendeka, kutoka Mamlaka hiyo ameeleza kuwa, watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa zote na kutaifisha vyombo vilivyohusika kubeba bidhaa hizo.

   
    “Tumeamua kufanya kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi na moja ya madhumuni ya kampeni hii ni kuwaonya wale wote wanaojihusisha na biashara za magengo kwani adhabu yake siyo tu kukamata bidhaa na kutaifisha vyombo bali pia kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa jela,” alisema Mahendeka.
   Pia amesema, mbali na wahusika hao wanaojihusisha na biashara za magendo kukwepa kulipa kodi ya Serikali, kuna uwekezekano wa kuwasababishia wananchi madhara ya kiafya kwa kuwa bidhaa zinazopita katika njia zisizo rasmi zinakuwa hazijathibitishwa na Mamlaka husika za Serikali.
   “Ni muhimu tukumbuke kwamba, bidhaa zote zinazopita katika njia za vichochoro au bandari bubu hazipiti katika utaratibu rasmi na hivyo zinakuwa hazijakaguliwa wala kuthibitishwa kama ni salama au la na Mamlaka husika kama vile TBS, TMDA, Mkemia Mkuu wa Serikali na nyinginezo. Kwa mantiki hiyo, bidhaa hizo zinaweza kuhatarisha afya za walaji,” alieleza.
      Hata hivyo,kampeni ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi imeanzia mkoa wa Dar es Salaam na timu ya maafisa wa TRA wanaendelea na kampeni hiyo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Mtwara na Lindi.

No comments

Powered by Blogger.