RPC Kingai Aieleza Mahakama ushahidi wa jamhuri
Kielelezo cha kwanza cha ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake, kimesomwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Kielelezo hicho kimesomwa leo Jumanne, tarehe 26 Oktoba 2021 na shahidi wa kwanza wa jamhuri katika kesi hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhani Kingai, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joackim Tiganga.
Akisoma kielelezo hicho ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa, ACP Kingai amedai yamechukuliwa katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala (RCO), iliyopo katika Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti 2020.
ACP Kingai amedai, katika maelezo hayo mtuhumiwa huyo alidai alikwenda Moshi mkoani Kilimanjaro na wenzake, kwa ajili ya kazi ya ulinzi maalum wa Freeman Mbowe na kwamba tarehe 25 Julai 2020, walipokelewa mkoani humo na wafanyakazi wa mwanasiasa huyo.
Amedai, katika maelezo hayo Kasekwa alidai baada ya kupokelewa Moshi, walipelekwa katika Hoteli ya Aishi ambako walionana na Mbowe, ambaye aliwaeleza kwamba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya anamsumbua, anatishia raia wa wilaya hiyo pamoja na kuwa na mpango wa kuiba kura.
Hivyo, hujuma za Sabaya zinampa wasiwasi yeye kupata ubunge na kuwa Mbowe aliwataka wamuwekee ulinzi Sabaya asifanikiwe ili apite njia nyeupe.
ACP Kingai ameendelea kusoma kielelezo hiko akidai, mtuhumiwa huyo alisema Mbowe aliwaelekeza wakamdhuru Sabaya kwa njia yoyote itakayowezekana ikiwemo kufuatilia nyendo zake katika maeneo anayopendelea kwenda hasa katika klabu za starehe Moshi na Arusha.
Shahidi huyo wa Jamhuri amedai, kupitia maelezo hayo ya onyo, mtuhumiwa alidai yeye na wenzake walipanga kumdhuru Sabaya kwa kutumia spray au perfume yenye sumu kwa kumwagia usoni.
ACP Kingai aliendelea kusoma maelezo hayo ya onyo, yaliyodai kwamba Kasekwa alidai baada ya kupewa maelekezo hayo, walianza zoezi la ufuatiliaji nyendo za Sabaya katika klabu za starehe ikiwemo klabu kubwa ya Koko riko ya jijini Arusha, lakini hawakumkuta, hivyo yeye na wenzake walirudi jijini Dar ea Salaam, kuendelea na majukumu mengine waliyopangiwa.
Kwa mujibu wa kielelezo hicho, ambacho Kimesomwa na ACP Kingai mahakamani hapo, Kasekwa na wenzake walienda Dar ea Salaam kuendelea na kazi nyeti, iliyodaiwa kuwa ni kulipua vituo vya mafuta na kufanya vurugu katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, ili kuonesha Serikali imefeli kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.
ACP Kingai amedai washtakiwa kwenye kesi hiyo walipanga kudhuru viongozi wa serikali, kufanya vurugu kwenye sehemu za watu wengi, kulipua vituo vya mafuta, kukata miti kwenye highway kuzuia magari yasipite hasa barabara ya Morogoro kwenda Iringa.
No comments
Post a Comment