Makamo wa Rais awapa maagizo mabalozi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, na kuwasisitiza kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazokwenda ambazo ni nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi.
Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amewataka Mabalozi hao kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.
Aidha amewaasa Mabalozi hao kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.
Amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kufanya jitihada za makusudi kuzifahamu vema nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania. Amesema katika kutekeleza diplomasia ya uchumi Mabalozi hao wanapaswa kuongeza ushirikiano na vongozi wa sekta binafsi ili kuwavutia kuwekeza Tanzania.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka msisitizo katika kuleta mabadilizo katika uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda hivyo amewasihi mabalozi hao kujielekeza katika kutafuta teknolojia rafiki zitakazosaidia katika kukuza na kuendeleza viwanda kulingana na mazingira ya hapa nchini.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaagiza Mabalozi hao Kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano hasa katika taasisi za utafiti na maendeleo.
No comments
Post a Comment