Header Ads

Header ADS

Mpiga debe mmoja auwawa kwa kisu wakigombania abiria huko kisamvu morogoro

Ugomvi uliozuka kati ya wapiga debe wa kampuni mbili za mabasi katika stendi kuu ya mabasi Msamvu mjini Morogoro, umesababisha kifo cha mmoja wao aliyechomwa kisu upande wa kushoto wa kifua na kufariki punde tu baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa morogoro.

 
Inadaiwa na mashuhuda kuwa wapiga debe hao waliokuwa wakigombea abiria, walianza kubishana wakiwa ndani ya stendi eneo linapoegeshwa mabasi, baadaye wakaamua kutoka nje na kuanza kupigana.
Mmoja wa mashuhuda hao, Sadick Zigwe alisema walidhamiria kupigana na walipotoka nje ya stendi hawakutaka wenzao waingilie ugomvi wao wakikisisitiza waachwe waonyeshane umwamba.
“Baada ya kupigana kwa muda mrefu mmoja alizidiwa na kuamua kutoa kisu na kumchoma mwenzake upande wa kushoto na kuanguka. Alikamatwa muda huo huo na askari, na baadaye tukapata taarifa kuwa amefariki,” alisema
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu, alisema tukio hilo lilitokana na ugomvi wa kugombea abiria kati ya Tazani Mndeme maarufu kama Sarange ambaye ni mkazi wa Mwembesongo na mpiga debe wa kampuni ya BM Coach na Abdallah Yassin, maarufu Hajamonga Bonge mkazi wa Kihonda na mpiga debe wa kampuni ya mabasi ya Abood.
Kamanda Muslim alisema ugomvi huo ulisababisha Yassin kumchoma kisu kifuani upande wa kushoto Mndeme ambaye alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na wakati akiendelea kupata matibabu alifariki dunia.
Alisema mtuhumiwa Abdallah amekamtwa na hatua za kumfikisha mahakamani zitafuata mara upelelezi utakapokamilik, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.
Walalamikia utaratibu
Kiongozi na msemaji wa kampuni ya BM, Joseph Mosha alisema mtafaruku uliotokea kati ya wapigadebe hao, unachangiwa na kukiukwa kwa mpangilio wa namna ya upakiaji magari ndani ya stendi, akisema yapo mabasi yanayoegeshwa eneo lisilo rasmi na kwamba wamekuwa wakitoa taarifa kwa wahusika.
Naye msemaji wa kampuni ya mabasi ya Abood Moris Masala alisema kama kampuni wamepokea kwa masikitiko kuhusiana na tukio hilo la uvunjifu wa amani.
Alisema wanachosubiri kwa sasa ni uchunguzi wa polisi pamoja na uongozi wa stendi, huku akisema walishawahi kufanya kikao kuhusu taratibu za upakiaji na uondokaji wa magari.
Mwenyekiti wa usafirishaji stendi ya Msamvu Aziz Kapilima, alisema kama uongozi wamesikitishwa na tukio hilo.
‘‘Kitakachofanyika ni kuhakikisha wanapata haki zao kwa kutosumbuliwa.Kwa stendi imekuwa ni dosari na tunajitahidi kudhibiti kwa kuzungumza na wapigadebe ili wapunguze jazba wanapotafuta abiria.’’ alisema.
Polisi
Kamanda Muslim aliwataka mawakala wa mabasi na wabipa debe kutogombea abiria wanaoingia stendi badala yake wawaelekeze katika mabasi ya kampuni zao kwa utaratibu.
Aliwataka kuacha kuingia na silaha ama vitu vyote hatarishi kama kisu, bisibisi. nyembe na sime, huku wahusika wote wakiwamo mawakala kuhakikisha wanatambuliwa kwa kuvaa sare na vitambulisho vya mabasi wanayofanyia kazi. Alisisitiza pia kuanza kwa upekuzi kubaini wanaoingia na vitu hatarishi.
Meneja wa Stendi ya Msamvu Kelvin Kilongola alipotafutwa mara kadhaa na waandishi wa habari alisema yeye si mzungumzaji kwamba watafutwe polis kwani ndio wenye uwezo wa kuzunguza mkasa huo.

No comments

Powered by Blogger.