Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesisitiza taasisi na Wadau kushirikiana katika kuhamasisha wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji hasa wajawazito na wagonjwa wanaopata ajali za mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani.
Prof. Makubi amesema hayo wakati alipotembelea kitengo cha maabara ya uchunguzi wa damu, kilichopo katika Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili ili kuongea na Watumishi na kujionea shughuli zinazofanywa katika kitengo hicho.
“Wagonjwa wetu wengi wanahitaji damu hasa wagonjwa wa Kansa na Selimundu, kwahiyo niwaombe mwendelee kushirikiana kukusanya damu lakini pia mtengeneze mfumo ambao utashirikisha Wadau wengine ili kuhamasisha wananchi kuchangia damu. ” Amesema Prof. Makubi.
Sambamba na hilo, Prof. Makubi amewataka uongozi wa Chuo kujikita katika ubora wa huduma pindi waendapo kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia muda mchache wa kukaa na mgonjwa, kurudisha mrejesho kwa mgonjwa na kauli nzuri pindi wanapohudumia mgonjwa.
Mbali na hayo, amewataka Wataalamu wa Afya kushirikiana katika kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali ili kurahisisha kupata suluhu ya changamoto kwa urahisi, huku akisisitiza kufanya hivyo kutarahisisha kuungwa mkono kutoka kwa Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali.
“Kwenye tafiti lazima mshirikiane, kwenye tafiti msiwe wachoyo, lakini vile vile tuzihusishe na idara nyingine, ni lazima tafiti mshirikiane, kwahiyo mkiwa katika muungano ni rahisi kuziunga mkono kama vile kuwatafutia fedha.” Amesema Prof. Makubi.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha katika kuendesha shughuli za tafiti na kuweka wazi kuwa, kuungana kwa pamoja katika kufanya tafiti kutarahisisha upatikanaji wa bajeti kutoka Serikalini.
Aidha, Prof. Makubi ametoa wito kwa Wataalamu wa afya kujiendeleza kwenye mafunzo ili kubobea katika taaluma zao jambo ambalo litasaidia kwa kiwango kikubwa katika kupambana na changamoto ya uhaba wa watumishi waliobobea katika taaluma hizo…
No comments
Post a Comment