FBI yazuia njama ya kuuawa kwa George W Bush
Shirika la FBI limefanikiwa kugundua na kuzia njama za kumuua rais wa zamani wa Marekani George W Bush iliyopangwa kufanywa na mfuasi mmoja wa kundi la Islamic State, mamlaka za Marekani zimesema.
Sasa yuko kizuizini na alifikishwa katika mahakama ya Ohio siku ya Jumanne.
FBI ilitumia taarifa za kichunguzi na ufuatiliaji wa kielektroniki ili kutatiza mpango wake.
Kulingana na hati za mahakama, mshukiwa huyo aliyetambuliwa kama Shihab Ahmed Shihab, 52 - ni raia wa Iraq ambaye amekuwa Marekani tangu 2020 na alikuwa na ombi lake la kuomba hifadhi ambalo liliwekwa pembeni kusubiri.
Katika mazungumzo na chanzo cha FBI, Shihab alisema alitaka kumuua Bush kwa "kuua Wairaq wengi" na "kuigawanya" Iraq.
Aliongeza kuwa anatumai kushiriki katika oparesheni hiyo binafsi "na hakujali kama angefariki, kwani angejivunia kuhusika".
Shihab alidaiwa kuviambia vyanzo alivyotarajia kuwatumia kusafirisha watu kwa njia ya magendo kuwa atawaleta wanachama wa Islamic State nchini Marekani, ingawa hashutumiwa kuwa mwanachama wa kundi hilo la kigaidi.
Katika tukio moja, Shihab na mmoja wa watoa habari walienda Dallas, Texas kuchukua video ya makazi ya Bush na Taasisi ya George W. Bush.
Machi 2022, alidaiwa kufanya mkutano katika chumba cha hoteli cha Columbus, Ohio kuangalia silaha na sare ghushi za polisi.
Sasa anakabiliwa na miaka 10 jela kwa kujaribu kuleta mtu kinyume cha sheria nchini Marekani, na mingine 20 kwa kusaidia jaribio la mauaji ya afisa wa zamani wa Marekani.
Msemaji wa Bush alisema rais huyo wa zamani "ana imani Huduma ya Siri ya Marekani na jumuiya zetu za kutekeleza sheria na kijasusi".
No comments
Post a Comment