Header Ads

Header ADS

Jamii ipewe elimu kuhusu anwani za makazi: KATIBU MKUU DKT. JINGU

 


Halmashauri kote nchini zimetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Anwani za Makazi na Postikodi katika maeneo yao.

kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu alipokuwa akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na Kyela kwa wakati tofauti alipofanya ziara yake ya kujionea maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo tarehe 18 Mei, 2022 Jijini Mbeya. 

Alieleza kuwa jamii inapaswa kupewa elimu ya umuhimu wa masuala ya anwani za makazi ili kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuhakikisha kila mmoja analibeba kwa uzito unaotakiwa.

“Endeleeni kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa anwani za makazi katika maeneo yenu, kwa kuzingatia faida zake ikiwemo kurahisisha shughuli za maendeleo,” Dkt. John Jingu

Aliongezea kuwa, ili kutatua changamoto za uelewa mdogo kwa jamii, aliwataka viongozi wa halmashauri kushiriki kikamilifu kwa kubuni mbinu mbalimbali zinazoendana na mazingira husika huku akiwataka kuendelea kuvitumia vyombo vya habari katika utoaji wa elimu hiyo.

“Hakikisheni mnavitumia vyombo vya habari vilivyopo katika jamii zetu ili kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja huku mkifanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha zoezi la Anwani za makazi linakamilika kwa wakati uliokusudiwa,” Dkt. Jingu

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Dkt. Vicent Anney aliahidi kuendelea kusimamia zoezi hilo ili kuendelea kuunga mkono jutihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika adhima yake ya kuiletea nchi maendeleo.

“Wilaya yetu imejipanga vizuri kusimamia zoezi la anwani za makazi, tunaahidi kutomuangusha Mhe. Rais wetu kwa kuendelea kutoa elimu kwa jitihada ili kila mwananchi aone umuhimu wa zoezi hili,”Alisisitiza Dkt. Anney.

Aliongezea kuwa zoezi likikamilika litarahisisha utekelezaji wa majukumu ya kiutawala katika ufuatiliaji na kujua taarifa za wananchi ambazo zitasaidia katika matukio mbalimbali yanapotokea.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa masuala ya anwani za makazi kwa Wilaya Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo Bw. Castory Makeule alisema Halmashauri imejipanga vyema ili kuhakikisha elimu inayafikia makundi yote yanayohusika na kurahisisha utekelezaji wake.

“Zoezi la ugawaji wa namba katika kata zote 29 limekamilika ikiwa ni sambamba na zoezi la uingizaji wa taarifa katika mfumo wa makisio ya taarifa 65,500 ambapo mpaka sasa jumla ya taarifa 67,685 zimeingizwa kwenye mfumo sawa na asilimia 101.77,”alisema Makeule

Aidha Halmashauri imeweza kuandaa nguzo/vibao 1000 zitakazowekwa katika barabara ndani ya Halmashauri ambapo kazi ipo katika hatua za mwisho ya ukamilishaji upakaji wa rangi na uandikaji wa majina ya mitaa na barabara.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Dkt. John Jingu akiangalia vibao vya namba za nyumba vilivyovyoandaliwa kwaajili ya zoezi la anwani za makazi Wilaya ya Kyela Jijini Mbeya.

No comments

Powered by Blogger.