MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais Samia Suluhu Hassan amemweleza kuwa ana nia thabiti ya kuendeleza demokrasia nchini ili kuwe na siasa za kistaarabu.

Profesa Lipumba alisema hayo baada ya kufanya mazungumzo  na Rais Samia, Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Na sisi hilo lilikuwa ndio kiu yetu, amesema kwamba suala zima la majadiliano, suala zima la mazungumzo ni kitu muhimu tujenge siasa za kistaarabu, tuweze kushindana kwa hoja, tueleze sera zetu na tuwe na uhuru wa kueleza sera zetu, lakini tufanye siasa za kistaarabu,” alisema.

Aidha Lipumba alisema Rais Samia alimweleza kuwa yeye ni muumini wa demokrasia na ana nia ya kujenga mifumo ya demokrasia ili kuwe na uhuru wa kujadiliana na kutoa maoni.

“Kazi yetu kama vyama vya upinzani na yeye alielewa hiyo pia ni kwamba kukosoa ni jambo jema kwa sababu kukosoa kunafanya watu waliopo ndani ya madaraka waweze kujirekebisha,” alisema.

Pamoja na hayo alimshukuru Rais Samia kwa kuwapa fursa ya kubadilishana mawazo na kumpongeza kwa kupewa jukumu la kuiongoza nchi.

Jana Rais Samia alimshukuru mwanasiasa huyo kwa kuhudhuria ziara yake mkoani Tabora.