Urusi Yadai Wanajeshi 959 wa Ukraine wamejisalimisha Mariupol
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema zaidi ya wanajeshi 900 wa Ukraine wamejisalimisha katika kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol.
Katika taarifa yake ya kila siku kuhusiana na mzozo huo, wizara hiyo imesema jumla ya wanajeshi 959 wamejisalimisha tangu Mei 16, 80 kati yao wakiwa wamejeruhiwa.
Wizara hiyo imesema wale wanaohitaji matibabu wamepelekwa katika hospitali moja iliyoko mji wa Novoazovsk unaodhibitiwa na Urusi.
Ukraine inatarajia kuwabadilisha wafungwa wa Urusi na wanajeshi hao waliojisalimisha ila Urusi haijathibitisha iwapo hilo litafanyika.
Mwezi uliopita, Urusi ilidai kuchukua udhibiti wa Mariupol baada ya wiki kadhaa za mashambulizi, ila mamia ya wanajeshi wa Ukraine walikuwa wamejificha katika mahandaki ya chini ya ardhi kwenye kiwanda hicho cha Azovstal.
Wizara ya ulinzi ya Ukraine inasema itafanya kila iwezalo kuwanusuru wapiganaji waliosalia kiwandani humo ambao idadi yao haijulikani kwa sasa, ila ikadai hawatofanya operesheni ya kijeshi.
No comments
Post a Comment