Header Ads

Header ADS

Maafisa Ugani wapatiwa mafunzo ya Upimaji udongo

Mtafiti Mkuu wa Udongo kutoka Chuo cha TARI  Uyole Mbeya Fedrick Mlowe akiwafundisha maafisa Ugani mkoani Ruvuma namna ya kupima udongo

 

 maafisa Ugani kutoka mkoani Ruvuma wakipata mafunzo ya upimaji wa afya ya udongo kwenye ukumbi wa Songea Klabu
MAAFISA Ugani 34 kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma wamepewa mafunzo ya  maandalizi ya upimaji wa afya ya udongo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu mjini Songea.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa wiki moja kutoka kwa  wataalam wa chuo cha TARI Uyole jijini Mbeya.
Akizungumza wakati  wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Emanuel Kisongo,amesema mafunzo hayo ya wataalam wa kilimo ngazi ya Kata na vijiji yatawajengea uwezo wa kutekeleza zoezi la upimaji wa udongo linalotarajia kufanyika katika vijiji 100 mkoani Ruvuma.
Ametoa rai kwa maafisa kilimo hao mara baada ya kufuzu mafunzo hayo wakasimamie na kutekeleza kwa weledi zoezi la upimaji wa afya ya udongo  katika vijiji ambavyo watapangiwa ambapo kila Afisa Ugani aliyepata mafunzo amepangiwa kufundisha vijiji vinne.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pikipiki 282 kwa ajili ya maafisa Ugani wa Kata na vijiji mkoani Ruvuma.
“Maafisa Ugani wa Kata na Vijiji wa Mkoa wa Ruvuma kila mmoja atapata pikipiki moja na seti ya  vifaa vya kutolea huduma  za ugani katika zoezi la kutambua afya ya udongo katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa’’.alisema Kisongo.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Udongo Kutoka  Chuo cha TARI –Uyole jijini Mbeya  Fredrick Mlowe  amesema zoezi hili lipo katika awamu ya tatu ya utekelezaji ambapo  awamu ya kwanza ilikuwa mikoa ya Mbeya na Songwe awamu ya pili ilikuwa mikoa ya Rukwa,Mbeya ,Iringa na Morogoro.
Mlowe ameitaja dhima ya mafunzo hayo kuwa ni kwa lengo la kujenga uelewa  wa afya ya udongo katika kanda sanjari na  kuzishauri kampuni za uzalishaji wa Mbolea kutoa mapendekezo ya mazao mbalimbali ili yaweze kuzalishwa kwa tija.
Mtafiti huyo amesema matokeo hayo yatawasaidia wazalishaji wa mbolea kutengeneza mbolea inayoendana na hali ya maeneo  kulingana na matokeo yaliyopatikana katika upimaji wa afya ya udongo.
Naye Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Martin Joseph akimwakilisha Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, amesema maafisa ugani waliopata mafunzo  watasaidia wakulima wa Mkoa wa Ruvuma  kujua matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kulima kwa tija.


No comments

Powered by Blogger.