Header Ads

Header ADS

Rushwa ya Ngono yanukia upangaji katika Vituo vya kazi

    Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imebaini upangaji wa vituo vya kazi kwa waajiriwa wa idara ya elimu katika halmashauri mkoani humo umegubikwa na viashiria vya rushwa ya ngono.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema Takukuru imefanya uchambuzi katika mifumo sita ukiwemo wa elimu na kubaini kuna uwepo wa mianya ya rushwa katika sekta ya elimu katika halmashauri mkoani humo.

Kibwengo alisema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utendaji wa taasisi hiyo ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu (Januari hadi Machi).
“Katika uchambuzi wa mfumo wa viashiria vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu ngazi ya halmashauri, tumebaini kuwa maeneo hatarishi ya uwepo wa rushwa ya ngono ni katika upangaji wa vituo vya kazi kwa asilimia 72,” alisema.
Kibwengo pia alisema eneo lingine hatarishi kwa uwepo wa rushwa ya ngono ni uhamisho wa walimu ndani ya halmashauri kwa asilimia 63.
Alisema Takukuru inaendelea na kampeni ya kuzuia rushwa ya ngono katika vyuo na taasisi nyingine kwa kutumia klabu za wapinga rushwa mkoani humo Kibwengo alisema taasisi hiyo imeendelea na kampeni ya kuzuia rushwa kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi 41 yenye thamani ya Sh bilioni 11.2 na kubaini miradi 10 ina upungufu ukiwemo wa vifaa vinavyotumika kuwa havikidhi ubora.
Alisema Takukuru imefuatilia miradi hiyo ya maendeleo katika sekta za ujenzi, elimu, afya na maji kwani ni mali ya wananchi na serikali inapeleka fedha nyingi. Kibwengo alisema, miradi hiyo inajumuisha miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19, ambayo serikali imetoa fedha nyingi.
“Kati ya miradi hiyo 41, 10 sawa na asilimia 24 ilikutwa ina upungufu kama wa kuchelewa kutekelezwa kwa mujibu wa mkataba, jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama, pia kuna matumizi ya vifaa visivyokidhi ubora na manunuzi kwa gharama zaidi ya bei ya soko,” alisema.
Kibwengo alisema katika kampeni ya kuzuia rushwa, Takukuru pia imeokoa Sh milioni 409.45 zilizolipwa kwa mkandarasi kinyume na taratibu katika utekelezaji wa mradi.


No comments

Powered by Blogger.