Header Ads

Header ADS

Walinzi Mbaroni kwa Mauaji ya Mwanakijiji .

 Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga linawashikilia walinzi wanne wa Kampuni ya Samu security waliokuwa wanalinda katika mgodi wa Eli - hilali uliopo Mwadui Wilayani Kishapu kwa tuhuma za kusababisha mauaji ya Hamisi Mayunga mwenye (27) mkazi wa Kijiji cha Dulisi wilayani humo
Inaelezwa walimpiga  risasi wakati akivua samaki kwenye bwawa lililopo ndani ya eneo la mgodi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga George Kyando, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa nne usiku katika eneo la mgodi wa El-Hilali, baada ya walinzi watano wa kampuni ya Samu Security kuondoka katika eneo lao la lindo walilopangiwa na kwenda kwenye bwawa la maji ambapo waliwakuta wananchi wakivua samaki na kuwataka kuondoka eneo hilo, huku mlinzi mmoja alifyatua risasi na kumpiga Mwananchi mmoja na kusababisha mauaji kisha alitelekeza silaha na kutokomea kusikojulikana
Kamanda Kyando amesema mlinzi aliyesababisha mauaji hayo anajulikana kwa jina la Emmanuel Chacha ambaye alitelekeza silaha nje ya kambi yao na kukimbia kusikojulikana na anatafutwa na jeshi la polisi ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Walinzi hao walikuwa watano kila mmoja alikuwa analindo lake alilopangiwa kulinda kwa siku hiyo lakini waliacha malindo yao na kwenda kwenye bwawa ambalo liko ndani ya mgodi huo na walipofika walikuta wananchi wanavua samaki waliwaambia waondoke wakati wakitoka alibaki Mwananchi mmoja ndipo mlinzi Emmanuel Chacha alifyatua risasi akasababisha mauaji”amesema Kamanda Kyando.
Katika hatua nyingine Kamanda Kyando amekemea tabia ya walinzi kutumia nguvu kubwa kwenye matukio ambayo hayahitaji bunduki,na kuwataka wamiliki wa makampuni ya ulinzi kuwachunguza vijana wanaowaajiri kama wanakidhi vigezo.
Hili ni tukio la pili kutokea la walinzi wa Kampuni binafsi kusababisha mauaji ya wananchi ambapo jeshi la polisi limeahidi kukutana na kampuni za ulinzi ili kuona namna ya kukomesha walinzi kutumia nguvu kubwa kwenye matukio madogo.



No comments

Powered by Blogger.