Watoto zaidi ya 262,039 kupatiwa Chanjo ya Polio Songwe
Wakati zoezi la kupatiwa chanjo kwa watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano likiendelea huko mkoani Songwe imeelezwa kuwa zaidi ya watoto 262,039 wanatarajia watapata chanjo ya awamu ya pili ikiwa ni vita ya kujikinga dhidi ya ugonjwa tishio wa polio uliothibitishwa katika nchi jirani ya Malawi mwezi februari, mwaka huu.
Hayo yamethibitishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Sidney Mdoe wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya chanjo ya polio uliofanyika katika Zahanati ya Mlowo wilayani Mbozi .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba amesema mkoa wa Songwe ni mkoa unaopakana na nchi mbili za Zambia na Malawi , hivyo amewataka wananchi kuwa makini na mwingiliano kwa kuhakikisha watoto wao wamepata dozi zote za polio zitakazotolewa na Serikali wakishirikiana na wadau mbalimbali.
"Pamoja na Mkoa kufanya vizuri na kuvuka lengo awamu ya kwanza ya Chanjo ambapo lengo lilikuwa kuwachanja watoto 224,455 lakini tulivuka lengo na kufanikiwa kuchanja watoto 262,039 sawa na asilimia 117, tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini kutokana na mwingiliano mkubwa na watu wa nchi jirani na watoto wengine kuzaliwa tuna amini idadi itaongezeka " Alisema Mkuu wa mkoa.
Kaimu Mganga Mkuu Sidney Mdoe alisema kabla ya uzinduzi walitangulia kutoa elimu kwa Wananchi hasa waliopo katika wilaya zilizopo mpakani ambazo ni Momba ambayo inapakana na nchi ya Zambia na Ileje inayopakana na nchi ya Malawi.
Alisema Kampeni ya uchanjaji itachukua siku nne kuwafikia wananchi wote ndani ya Mkoa wa Songwe.
"Mkakati uliopo ni kuhakikisha watoto wanakamilisha chanjo zote nne za polio ambapo hii ni chanjo ya pili kwa mkoa wetu, hivyo tutabakiwa na chanjo mbili ambazo tutazifanya kwa Muongozo wa Wizara ya afya" Alisema Mdoe.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ofis ya Rais Tamisemi idara ya afya Silvery Maganza alisema Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa minne ambayo inapakana na nchi ya Malawi, Hivyo unapewa kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha watoto wote wanapewa chanjo.
Aliitaja mikoa mingine ambayo inapata chanjo kwa awamu ya pili kuwa ni Njombe, Mbeya na Ruvuma.
"Awamu ya kwanza iliyofanyika katika mikoa minne tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafikia watoto wengi na kuvuka lengo kwa kufikia asilimia 117 , awamu hii ya pili tunategemea kuwafikia watoto zaidi ya milioni kumi (10) kwa upande wa Tanzania bara na Visiwani " alisema Maganza.
Baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamepata chanjo wamesema watahakikisha watoto wao wanapata chanjo zote nne za polio kama zilivyotangazwa na Serikali Ili watoto wao waweze kuwa salama.
Rehema Mwampashi Alisema kabla ya kupewa chanjo walipewa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo , na kudai kuwa atazingatia kuhakikisha mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili anapata chanjo zote nne kulingana na maelekezo ya watalaam.
No comments
Post a Comment