Raia mmoja wa Ethiopia na baba wa watoto 11 amekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii nchini humo baada ya kujiunga na chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 69.

Akiwa yatima katika umri mdogo, Tadesse Ghichile, hakuweza kuendelea na elimu rasmi baada ya kumaliza shule ya sekondari.

Sasa, anahudhuria masomo ya Chuo Kikuu cha Jimma kilichopo sehemu ya magharibi ya nchi ambako anatarajia kuhitimu na shahada ya matibabu.

Tadesse Ghichile ni mkulima. Asipokuwa shambani, hufanya kazi kwenye mgahawa katika kijiji chake ili kutunza familia yake.

Lakini alipata muda wa kufanya na kufaulu mtihani wa kitaifa wa kuingia chuo kikuu.

Miaka 10 iliyopita ndipo alipoamua kurudi katika elimu yake rasmi ambayo aliiacha akiwa darasa la nane kufuatia kifo cha wazazi wake.

Kwa muda mrefu alikuwa amepata ugumu kurudi shuleni haswa baada ya kuanzisha familia. Lakini mara tu aliporudi, alidhamiria kumaliza hadi mwisho.

Sasa, amejiandikisha katika moja ya chuo kikuu kikubwa zaidi nchini humo. Aliiambia BBC kuwa amekuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wanafunzi wenzake katika miaka michache iliyopita na kwamba anatazamia kile kitakachotokea mbeleni.