Header Ads

Header ADS

Wiki ya Sanaa na ubunifu yazinduliwa rasmi Dodoma

 Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu (MAKISATU)yanayofanyika mwaka huu Kitaifa yataibua zaidi ubunifu na teknolojia zitakazojibu na kufumbua changamoto za kiuchumi na kijamii wanazokabiliana nazo wabunifu katika shughuli za kila siku.


Hayo yamezungumzwa na  Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman  wakati akifungua rasmi wiki ya Ubunifu jijini Dodoma  na kusema kuwa wiki hii itaonesha bunifu mbalimbali ambazo zimebuniwa na Watanzania kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kila siku.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira na kutoa fursa ya kuweza kuibua wabunifu zaidi na kuwaendeleza kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo na kuimarisha maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

“Serikali inatambua umuhimu wa wiki hii na ndio maana maonesho haya yanafanyika ili kuendelea kuibua na kukuza vipaji tunapaswa kufanya maonesho naamini itatusaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa,” amesema Othman.

Pamoja na hayo amesema Mbali na kusaidia ukuaji wa uchumi kwa taifa ubunifu pia utatoa mchango katika upatikanaji wa ajira pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni kuweza kutoa fursa za ajira kwa wenyeji kutokana na ujuzi walionao.

“Kwa hivyo, na sisi tutachukua kila hatua kuona malengo yetu ya kuhamasisha ubunifu na teknolojia yanafanikiwa, ameongeza.

Hata hivyo amesema Serikali zote mbili zimeazimia kujenga uwezo wa ndani kwa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu, miundo mbinu na vifaa vya kisasa vya utafiti na ubunifu pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya Taasisi za Sayansi na Teknolojia pia sekta ya viwanda.

“Matunda ya jitihada za Serikali, katika utekelezaji wa malengo hayo na hatua zinachukuliwa yote yanabainika kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu,” amesema.

Katika kuhakikisha ubunifu na elimu ya Sayansi na Teknolojia inawekezwa kwa vijana ili kupata wataalamu wa fani mbali mbali, kwa upande wa Zanzibar wameanzisha Mradi wa kujenga vituo 22 vya ubunifu wa Sayansi Unguja na Pemba. Vituo hivyo, vimeanza kutumika ambao ni mradi uliogharimu USD Milioni 35 zikiwa ni Mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Vile vile, jitihada za kuimarisha vituo vya mafunzo ya amali kote nchini zinaendelea ili kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi wa fani mbali mbali kwa lengo la kupunguza changamoto ya ajira.


Pia Mhe.Othman ametoa pongezi kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa jitihada zao katika kusaidia usimamizi wa tafiti mbali mbali nchini na kuzishauri Serikali zetu kuhusiana na masuala yanayohusu Sayansi, Ugunduzi na Teknolojia kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu.

“Serikali itaendelea kuijengea uwezo wa kifedha na kitaalamu COSTECH, ili iweze kusaidia zaidi shughuli za utafiti na ubunifu nchini kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesema Mhe.Othman

Ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa Maonesho ya Wiki ya Ubunifu Kitaifa kwa mwaka huu wa 2022 huku ikiwa na kauli mbiu isemayo “Ubunifu kwa maendeleo endelevu”

No comments

Powered by Blogger.