Mkazi wa kijiji cha Marumba kata ya Marumba wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Lumba Amanzi, amefariki Dunia baada ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali ya mwili wake na Tembo.
Mjane wa marehemu Lumba Amanzi kulia akipokea mkono wa pole( rambirambi) ya Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro aliyekwenda katika familia hiyo kufuatia kifo cha Mzee Lumba Amanzi aliyeuawa na Tembo.
Tukio hilo
limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita,ambapo marehemu alipatwa na mkasa
huo wakati akitoka shambani kuelekea kijijini kwa ajili ya kwenda kuswali swala
wa Ijumaa.
Kwa mujibu wa
mjukuu wa marehemu Said Halumba ni kwamba,marehemu alikuwa anaoga katika mto na
ghafla alitokea Tembo mmoja aliyekwenda kwa ajili ya kunywa maji katika
mto huo na kuanza kumshambulia.
Alisema, licha
marehemu kujitahidi kukimbia kwa lengo la kuokoa maisha yake lakini alizidiwa
mbio na Tembo huyo ambaye alimwangusha chini kumkanyaga sehemu mbalimbali na
kufariki papo hapo.
Halumba ameishukuru
Serikali kwa msaada uliotoa kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya
marehemu,hata hivyo ameiomba kupeleka askari wa Wanyamapori wengi kata ya
Marumba ili kukabiliana na Tembo na wanyama wengine wakali na waharibifu.
Mwenyekiti wa
Serikali ya kijiji cha Molandi kinachopakana na Marumba Mohamed
Manjolo,ameiomba Serikali kupeleka askari katika kata ya Marumba ili
kurudisha hali ya usalama kwani kama Tembo wataendelea kuachwa bila
kudhibitiwa kuna hatari ya wananchi kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo
kwa ofu ya kukutana na tembo.
Alisema,Tembo hao
wanaotembea makundi makundi wanatoka katika Hifadhi ya Taifa ya Selou na mapori
yaliyohifadhiwa kwa ajili ya uhifadhi wa misitu wamekuwa wakiharibu mazao
mashambani na kuleta taharuki kubwa kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya
Tunduru Julius Mtatiro ambaye alifika nyumbani kwa marehemu kwa lengo la kuipa
pole familia iliyompoteza mpendwa wao alisema,serikali imeshapeleka
askari wa Wanyamapori ambao wameanza kazi ya kuwafukuza Tembo hao
ili warudi katika maeneo yao.
Mtatiro ambaye ni
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tunduru,amewataka wananchi
wa kijiji hicho na maeneo mengine kuchukua tahadhari wanapokwenda shambani na
kwenye shughuli nyingine pindi wanapoona dalili za kuwepo kwa wanyama wakali.
“tumetoka makao
makuu ya wilaya kuja apa Marumba kwa ajili ya kushiriki pamoja nanyi majonzi
haya makubwa mliyopitia kama familia ya kumpoteza mzee wa familia hii
Lumba Amanzi,lakini mimi nilikuwa safari ya kikazi nje ya Tunduru lakini
niliwatuma baadhi ya viongozi wengine kuja kushiriki kwenye msiba huu
mkubwa”alisema.
Alisema, serikali
ina wajibu wa kushiriki na kuwa bega kwa bega inapotokea misiba ya watu
kuvamiwa na Tembo na wanyama wakali ambao wamekuwa tatizo kubwa katika maeneo
yetu.
Alisema,kutokana na
tatizo la watu kuvamiwa na kuuawa na wanyama wakali,serikali imeanza ujenzi wa
kituo kikubwa cha askari wa wanyama pori ambao watakuja kwa ajili ya
kukabiliana na wanyama hao.
Mtatiro,amemwagiza
Afisa tarafa wa Nalasi na viongozi wa ngazi ya kata na kijiji kuhakikisha
wanakuwa karibu na familia hiyo kwa lengo la kufahamu matatizo
ikiwamo watoto kushindwa kwenda shule kwa kukosa sale na mahitaji mengine
muhimu ili maisha yaweze kuendelea kama awali.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro akipika ugali wakati alipotembelea familia ya marehemu Halumba Amanzi aliyeuawa na Tembo wakati akitoka shambani mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro akizungumza na baadhi ya wanandugu wa familia ya marehemu Lumba Amanzi aliyeuawa na Tembo,Mkuu huyo wa wilaya alikwenda kwa ajili ya kuwapa pole familia hiyo kwa kumpoteza ndugu yao ambaye ndiyo alikuwa kiongozi wa familia hiyo.
No comments
Post a Comment