Mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Hamis Hassan, mkazi wa Kijiji cha Kambuzi, Kata ya litapuga wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kwa tuhumu za kuiba debe mbili za mahindi.

Inaelezwa kuwa kabla ya tukio hilo la mauaji, wananchi walimtuhumu marehemu kuiba debe mbili za mahindi mali ya Emmanuel Malela lakini kiongozi wa mtaa huo aliwaagiza watu wanaomshikilia wamfikishe kituo cha polisi Kanoge ila wakajichukulia sheria mkononi.

Watu watano wanaotuhimwa kutekeleza mauaji ya Hamisi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na kupitia kitengo cha upelelezi walibainika kukimbilia mkoani Tabora na kurudishwa Katavi kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayowakabili.