Brela Yaanika Mafanikio Ya Kusajili Makampuni Kipindi cha Rais Samia
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Tanzania (BRELA) umesema kumekuwa mwitikio mkubwa wa watu kusajili Makampuni,Majina ya Biashara sambamba na kupata leseni za biashara zao tokea Rais Samia Suluhu alipoingia madarakani.
Hayo yalisemwa na Msajili Msaidizi kutoka Brela Seleman Seleman wakati wa
maonyesho ya 9 ya biashara na utalii yanayofanyika jijini Tanga ambapo wamekuwa
wakitoa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kusajili biashara zao.
Alisema kwa kipindi kimoja tokea Rais Samia aingie madarakani wameweza kusajili
makampuni 11422 ambapo wameweza kusajili majina ya biashara 22251 lakini pia
alama za biashara wamesajili 3056 ambapo katika leseni za kundi A wametoa
leseni 12704.
“Kwa kipindi hiki kimoja cha mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan
kimeonyesha mafanikio makubwa ukilinganisha na vipindi vingine jambo ambalo
limeonyesha ari kwa watu kusajili makampuni, majina ya biashara lakini pia
kupata leseni za biashara zao, “alisisitiza Seleman.
Aidha amesema hali hiyo pia imewaongezea ari wao kama watendaji wa Brela ambapo
kupitia matamasha mbalimbali wanashiriki ili kuifikia jamii ambapo walengwa
wakiwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
“Wito wangu kwa wafanyabishara kabla ya kuanza kufanta jambo wawe wanapitia na
kutafuta taarifa kwanza kwa wahusika ambao ni Brela kupitia mitandao ya kijamii
au website zetu zinazoeleza sisi tunafanya nini na ikiwa kama kuna sehemu mtu
hajaelewa kuna namba ya huduma kwa wateja hivyo watu wanaweza kupiga na kupata
taarifa sahihi hii itawapunguzia wateja kupewa taarifa na watu ambao si sahihi,
“alibainisha Seleman.
Wakizungumza katika banda hilo baadhi ya wakazi wa jiji la Tanga waliotembelea
akiwemo Richard Otto alisema alilazimika kufika hapo ili aweza kujua namna ya
kusajili jina la biashara na kampuni kwa kuwa alikuwa hajui umuhimu wa kusajili
biashara yake.
Aidha alisema wanachonufaika nacho baada ya kufika hapa Brela ni kurasimisha
biashara hasa kwa vijana ambao wamekuwa wakifanya biashara bila kusajili na
hivyo kushindwa kutambulika.
“Tunashukuru tumepata suluhisho njia za kufanya mwanzoni huu mfumo
ulikuwa unasumbua pale ulipoanzishwa mfumo wa usajili online lakini sasa ivi
nimeambiwa taratibu zimekaa vizuri, “Alisema, Otto.
Hata hivyo kwa upande wake mkazi wa Korogwe ambaye alitembelea banda hilo
Veronica Temu alieleza kufurahishwa na uwepo wa wakala huo kwenye maonyesho
hayo kwamba utawasaidia kufanya usajili wa biashara zao ikiwemo kutumia simu
zao au kompyuta akiwa nyumbani kwake na hivyo imewarahisishia kwa kiwango
kikubwa.
No comments
Post a Comment