Matapeli wa mtandao wakamatwa Dar, wakiwemo wanaojifanya mawakala wa Freemason
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia
watu 23 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utapeli kwa njia ya mtandao.
Kukamatwa kwa watu hao ni matokeo ya oparesheni maalum
iliyofanywa na kanda hiyo kwa kushirikiana na timu maalumu ya Kuzuia na
Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni.
Operesheni hiyo iliyofanyika kati ya Mei 18 hadi Juni 26
ilifanyika pia katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro ambapo watuhumiwa
wengine walikamatwa huko.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema waliokamatwa ni watuhumiwa waliokuwa wakijifanya wakuu wa shule, waganga wa kienyeji, ndugu wa waathirika, wahudumu wa makampuni ya simu au mawakala wa Freemason.
Amesema watuhumiwa hao huwatumia watu ujumbe mbalimbali
kupitia namba tofauti za simu na kujifanya wanania ya kusaidia watu badala yake
huishia kuwaibia.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Julius Simon Mwabula (20) ambaye
ni mkazi wa Ifakara Morogoro sambamba na wenzake 22.
Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo
wanavitumia kufanya uhalifu huo ikiwemo hivyo ni kama Kompyuta mpakato 2,
kompyuta ya mezani 1, simu za aina tofauti 28, flash 2, modem ya mitandao yote
na kadi za simu za mitandao mbalimbali zaidi ya 50.
Katika operesheni hiyo wamekamatwa pia wanawake wawili kwa
kosa la kufanya biashara ya ngono mtandaoni na kusambaza picha za utupu kwenye
mitandao ya kijamii.
No comments
Post a Comment