Wakuu wa shule waaswa kuhusu matumizi ya fedha zitolewazo na serikali
Walimu wakuu wa shule zote nchini wametakiwa kusimamia ipasavyo miradi
yote inayotekelezwa na serikali katika shule zao ikiwemo kuhakikisha fedha
zinazoletwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutimiza azma ya serikali
ya kuboresha sekta hiyo.
Aidha wameagizwa kusimamia vizuri nidhamu ya
walimu na wanafunzi, kutoa motisha chanya kwa walimu na wanafunzi wao
wanapofanya vizuri katika masomo yao na kuwa viungo vizuri kwenye jamii
inayowazuguka.
Maagizo hayo yametolewa jana na Katibu Mkuu
wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Profesa Riziki Shemdoe
alipokuwa akihitimisha semina ya utendaji kwa Wakuu wa shule za sekondari zenye
kidato cha 5 na 6 na Maofisa Elimu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara iliyofanyika
Mjini Tabora.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa
utawala wa Rais Samia, fedha nyingi zimeletwa katika shule mbalimbali kwa ajili
ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni na
ununuzi wa thamani.
Alibainisha kuwa haya yote yalilenga
kuboresha miundombinu ya shule hizo ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na
ufundishwaji, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuinua kiwango cha elimu.
‘Hakikisheni miradi yote inasimamiwa ipasavyo
na fedha zinazoletwa zifanye kazi iliyokusudiwa, ninyi ndiyo mko karibu na
watekelezaji miradi hiyo, msaidieni Mheshimiwa Rais, kinyume na hapo
tusilaumiane’, alisema.
Profesa Shemdoe alisema zaidi ya shule 300
zimejengwa katika wilaya na majimbo yote ikiwemo kila kata ili kuhakikisha
watoto wote wanaofaulu darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga kidato cha 1,
hivyo akawataka kuzisimamia.
Alisisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yao ni
kusimamia sekta hiyo ili yale yote yanayofanyika yalete tija kubwa huku
akibainisha kuwa jamii iliyoelimika na kupata ujuzi ndiyo msingi mkuu wa maendeleo
ya taifa lolote.
Aliwataka kuhakikisha mazingira ya shule zao
na miundombinu vinatunzwa vizuri ili viendelea kuwa bora huku akiwataka kuweka
utaratibu mzuri wa kurekebisha miundombinu inapoharibika ili kutoathiri
ufundishaji na ufundishwaji watoto.
No comments
Post a Comment