Bil 15 zatengwa na serikali kuimarisha ushirika nchini
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan
imetenga kiasi cha sh bil 15 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023 ili
kuimarisha shughuli za vyama vya ushirika nchini na kuinua wakulima.
Hayo yamebainishwa jana na Naibu Waziri wa
Kilimo Anthony Mavunde alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika
Duniani (SUD) ambayo yanafanyika Kitaifa katika viwanja vya Nane Nane vilivyoko
Ipuli Mjini Tabora.
Alisema dhamira ya serikali ni kuinua vyama
vya ushirika na kukuza sekta ya kilimo kutoka asilimia 4 ya sasa hadi 8 na
kufikisha asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 lengo likiwa kupanua wigo wa
uzalishaji ili kumnufaisha zaidi mkulima.
Alibainisha kuwa ili kufanikisha lengo hilo
serikali imeongeza bajeti kuu ya Wizara hiyo kutoka sh bil 294 hadi bil 954
huku bajeti ya kuinua ushirika pekee ikiongezeka kutoka sh bil 12 hadi 15
katika mwaka huu wa fedha.
Naibu Waziri aliongeza kuwa Wizara yake
imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo inavutia wadau wengi zaidi ikiwemo
kukuza uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla, kupunguza umaskini, kutengeneza
ajira na kuanzishwa mashamba makubwa (block farm10,000 ).
Alisisitiza kuwa ushirika ni nyenzo muhimu
sana hivyo akamtaka Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Ushirika kuelimisha jamii juu ya manufaa ya ushirika ili usiharibiwe kuondoa
dhana hasi miongoni mwa watu juu.
‘Naipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na
Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini kwa kazi nzuri mnayofanya kusimamia na
kuelimisha jamii juu ya manufaa ya kujiunga kwenye ushirika’, alisema.
Aliongeza mikakati mingine ya Wizara hiyo
kuwa ni kuongeza uzalishaji wa mbegu ambapo wanatarajia kutumia kiasi cha sh
bil 43, kuboresha miradi ya umwagiliaji kwa sh bil 361 na kuhifadhi mazao
ya wakulima.
Mavunde alielekeza Tume ya Maendeleo ya
Ushirika, Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) na Chuo Kikuu cha
Ushirika (MUCCOBS) kuendelea kutoa mafunzo ya usimamizi vyama vya ushirika,
utunzaji nyaraka na uendeshaji shughuli zao ili kuwaongezea
ufanisi.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu
wa wilaya ya Tabora Dkt Yahaya Nawanda alisisistiza kuwa wataendelea kuhimiza
uanzishwaji vyama vya ushirika kutokana na umuhimu wake kwa jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mkoani hapa Hassan Wakasuvi alipongeza serikali kwa kutekeleza ilani ya
uchaguzi kwa vitendo katika kuimarisha ushirika hapa nchini ili kuwainua
wakulima.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo
ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege alibainisha kuwa maadhimisho hayo ni
muhimu sana kwani wanaushirika watapata fursa ya kuonesha kazi zao na kujifunza
mambo mbalimbali kutoka kwa wenzao.
No comments
Post a Comment