Neema yawashukia wasanii Tanzania: waahidiwa kufunguliwa milango zaidi soko la Hollywood
Wasanii mbalimbali wa
Tanzania hasa wa muziki na filamu wameahidiwa kufunguliwa milango zaidi katika
soko na kiwanda kikubwa zaidi duniani cha burudani cha Hollywood nchini
Marekani ili kupata mafanikio zaidi katika kazi zao.
Ahadi hiyo imetolewa na
mmoja wa watendaji na wawekezaji wa masuala ya sanaa na burudani nchini
Marekani, Bw. Tyrone Davis, alipokutana na kufanya mazungumzo ya kina na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka nchini Tanzania, Dkt. Hassan
Abbasi, siku ya Jumanne Juni 28, 2022, jijini hapa.
Pamoja na sasa kujikita
zaidi katika kampuni za fedha na masuala ya teknolojia nchini Marekani akiwa
Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Urban Icon na pia Mwenyekiti wa taasisi ya kifedha
ya IN CARD, Bw. Davis anabaki kuwa mmoja wa wadau wakubwa wa Hollywood.
Katika miaka yake ya
takribani miaka 20 katika kiwanda cha Burudani nchini Marekani, Bw. Davis
anaendelea kubaki mmoja wa watu wanaofahamiana na kila mdau muhimu wa Hollywood
akiwa amefanya kazi na wasanii nguli wa zamani kuanzia MC Hammer, Lionel Richie
na produza mwenye tuzo 38 za Grammy, Bw. Quincy Jones, miongoni mwa wasanii
wengine wengi.
“Wasanii wa muziki wa
Tanzania wanavipaji hivyo wanapaswa kutafutiwa namna ya kuingia zaidi katika
soko kubwa kama la Hollywood kuanzia fursa za kurekodi na wasanii wakubwa,
kusainiwa na rekodi kubwa ili waendelezwe na kukua zaidi hadi kushirikishwa
katika matamasha makubwa.
“Kwa wale wa filamu ni
muhimu nao washiriki filamu kubwa na sisi diaspora tulioko huku turudi katika
nchi kama Tanzania na kuwekeza miundombinu ya kisasa ya sanaa kama studio.
Kupitia kampuni na mitandao yangu tutafungua njia hiyo kwa kuratibu pamoja
programu ya kimkakati pamoja na Serikali ya Tanzania,” aliahidi Bw. Davis.
No comments
Post a Comment