Mfanyabiashara adaiwa kupora nyumba na kumteka mfanyakazi wake kwa miaka 10
Mfanyabiashara mmoja maarufu wa
mjini Singida anadaiwa kumteka na kumficha kusikojulikana kwa zaidi ya miaka 10
mtu mmoja aliyekuwa mfanyakazi wake na haijulikani kama yupo hai au amefariki.
Madai hayo yalitolewa na Omari
Rashid mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge, kwenye mkutano wa
kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani
Manispaa ya Singida.
Aliongeza kuwa mfanyabiashara
huyo (anamtaja jina) alimrubuni baba yao kwamba atamlea na familia yake kwa
kipindi chote cha maisha yao lakini katika hali ya kushangaza wamejikuta wakitimuliwa
na mfanyabiashara huyo ambaye amejimilikisha nyumba yao iliyopo eneo la Majengo
Manispaa ya Singida.
“Mheshimiwa RC utatusaidiaje
jambo hili ili tupate nyumba yetu natujue hatma ya baba yetu alipo,” alisema.
Kufuatia ombi hilo, Mkuu wa
Mkoa Singida, Dk.Mahenge alimwagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida ( DAS)
na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Lucas Mwakatundu wachukue maelezo ya kina ya mlalamikaji huyo ili serikali iweze
kuyafanyia kazi madai yake.
Aidha, Dk.Mahenge aliwagiza
viongozi kuanzia ngazi za wilaya hadi chini kujenga tabia ya kuitisha mikutano
ya wananchi na kusikiliza kero zao.
Alitumia nafasi hiyo
kuwaeleza wananchi mafanikio mbalimbali yaliyofanywa na serikali ya awamu sita
chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
No comments
Post a Comment