Gesi yamuua mwalimu Morogoro, polisi watilia shaka
Mwalimu wa shule ya sekondari Morogoro, Daudi
Senyagwa amefariki baada ya nyumba aliyokuwa akiishi mtaa wa Seminari
kata ya Kingoluwira manispaa ya Morogoro kuteketea kwa moto tukio ambalo polisi
wamelitilia shaka.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo balozi wa
nyumba kumi katika eneo hilo, Gregory Tandu amesema saa tano usiku
alipigiwa simu na jirani yake kuwa nyumba ya jirani yao kuna moto na alipofika
alishuhudia moto na gari ndogo ya mwalimu ikiwa imeegeshwa nje.
"Hakukuwa na dalili ya mtu yeyote kuzunguka eneo
hili, tukampigia simu mwenyekiti ambaye aliwapigia simu polisi kuwaarifu
moto ulikuwa mkubwa na kulikuwa na dalili kama ya mlipuko," amesema.
Mwenyekiti wa chama cha walimu manispaa ya Morogoro,
Gaspar Jaka amesema wamepokea taarifa za tukio hilo kwa masikitiko
ikizingatiwa mwalimu huyo alikuwa mwadilifu na mchapakazi.
"Mwalimu alikuwa anafundisha somo la Jiografia
sekondari ya Morogoro, kifo chake kimetutia simanzi kubwa sana na pengo lake
sio rahisi kuzibika,"amesema Jaka.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Morogoro,
Ralph Meela aliyefika eneo la tukio amesema taarifa za awali zinaonesha kifo
cha mwalimu huyo kimesababishwa na gesi.
Hata hivyo, amesema wana mashaka na tukio hilo kutokana
na kukuta mlango wa nyumba ya mwalimu ukiwa wazi huku funguo wa nyumba
zikining'inia kwenye kitasa nje ya mlango.
No comments
Post a Comment