Mauaji ya mapadri Askofu Nkwande afunguka
Askofu wa Jimbo Katoliki Mwanza, Renatus Nkwande
ameziomba taasisi za elimu na dini nchini kufundisha upendo ili kuondoa
ubinafsi, ukatili na roho ya mauaji inayosababisha vifo vikiwemo vya mapadri
nchini.
Akizungumza jijini Mwanza katika maadhimisho ya siku
ya somo ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Askofu Nkwande
alitaja sababu nyingine ya mauaji nchini kuwa ni jamii kukosa hofu ya Mungu.
Ameziomba taasisi za elimu na dini nchini kuhimiza
upendo, kujaliana, kudhibiti uhuru uliopindukia huku akiitaka jamii kuachana na
ukatili unaosababisha roho ya mauaji.
"Tunapaswa kujilea na kujilinda katika taasisi za
elimu ya juu na kati ndiyo mahala ambapo mbali na taaluma, pia mtu anafundishwa
maadili ya kumuheshimu na kumuogopa Mungu," amesema Askofu Nkwande.
Awali, makamu mkuu wa Saut, Profesa Costa Mahalu amesema
ili kuhimiza maadili katika jamii kila mwanafunzi katika chuo hicho
anafundishwa kozi ya maadili ya jamii ili kumfanya ajitambue, upendo na
kuithamini jamii.
Amesema ili kuziishi falsafa za Padri Augustino wa Hippo
ambaye jina lake kilipewa chuo hicho, chuo kimekuwa kikitoa mafunzo na semina
mara kwa mara kwa wanachuo ili kutambua wajibu wao kwa jamii.
"Tunawahamisha wanachuo wetu kuziishi ndoto za
Mtakatifu Augustino ikiwemo upendo kwa sababu chuoni ni sehemu ya malezi na
makuzi kwa vijana. Tusipende kuwahujumu watu bali tuwe wapenda haki,"amesema
Profesa Mahalu.
Mtakatifu Augustino wa Hippo alizaliwa mwaka 354 baada ya
kuzaliwa kwa Yesu na maadhimisho ya kumkumbuka yakifanyika jana na
wasomi, viongozi wa dini na wanafunzi zaidi ya 660 wa chuo hicho kushiriki.
Matukio ya mauaji ya mapadri
Juni 11, 2022 Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Mbeya, Michael Samson wa Shirika la Wamisionari wa Afrika alidaiwa kuuawa baada
ya mwili wake kukutwa katika mto Meta maeneo ya Sabasaba jijini Mbeya.
Aprili 15, 2022 Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano,
Padri Francis Kangwa (49) aliuwawa na mwili wake kukutwa katika tenki la maji
lililokuwa nyuma ya makazi ya mapadri katika mtaa wa Ottoman jijini Dar es
Salaam.
No comments
Post a Comment