Wahariri wa Redio za jamii watakiwa kuielimisha jamii kuhusu Sensa
Wahariri wa Radio Jamii hapa nchini wametakiwa
kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu na kuhamasiha wananchi ili waweze
kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Akizungumza leo juni 16 2022 wakati wa ufunguzi wa siku ya kwanza ya mafunzo kwa wahariri wa Redio Jamii yanayofanyika mjini Iringa kwa siku mbili, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Said Ameir amesema kuwa wahariri hao wanalo jukumu kubwa katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wote ili washiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi Agosti 23, 2022.
Bw.Ameir
amesema kwamba amekutana na wahariri hao ikiwa ni muendelezo wa kutoa mafunzo
kwa watu wa habari, ili kuhakikisha zoezi la sensa linafanikiwa kwa watu wote.
" Baada ya mkutano na Wamiliki wa
Vyombo vya Habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, tumefanya mafunzo kwa
Wahariri wa Mitandao ya Kijamii na sasa Wahariri wa Redio za Kijamii",
alisisitiza Bw. Ameir.
Akieleleza zaidi amesema kuwa mafunzo
kwa makundi mbalimbali ya wadau ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Uelimishaji na Uhamasishaji.
Kwa upande wake mmoja wa watoa mada
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hellen Hilary amesema Sensa ya Watu na
Makazi itasaidia Serikali kupanga mipango ya Maendeleo kwa kuzingatia takwimu
zitakazokusanywa.
Baadhi ya mada zitakazotolewa kwa
Wahariri hao ili kuwajengea uwezo ni pamoja na; Sensa na Sheria ya Takwimu,
Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na Maandalizi yake, Sensa na Mbinu za
Uripoti kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na Matumizi ya Mitandao ya
Kijamii.
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika
Agosti 23, 2022 kote nchini ikilenga kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo.
No comments
Post a Comment