Jeshi la polisi Simiyu limetakiwa kudhibiti wizi na unyang’anyi
unaoendelea katika magari ya abiria almaarufu ‘Michomoko’ siku za jumanne na
alhamisi.
Agizo hilo limetolewa na Baraza la Madiwani katika Halmashauri
ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wakati wa Mkutano wa kujadili taarifa za robo ya tatu
(mwezi Januari-March), uliofanyika Bariadi Sekondari, ambapo madiwani hao
wamesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiporwa pesa zao kwenye magari na watu
wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja amesema Unyang'anyi
huo umekuwa ukifanyika siku za Jumanne na Alhamisi ambapo magari mengi hufika
mjini Bariadi na Dutwa mnadani.
"Wananchi wa Old Maswa wanatekwa na wenye magari yanayokuja
mnadani, wanakabwa, wanapigwa makofi na kunyang'anywa fedha zao...tunaomba
Jeshi la Polisi kudhibiti hali hii" amesema Masanja.
Mwenyekiti huyo amelitaka Jeshi la Polisi kuweka mitego maalumu
ili kuhakikisha wanakamata wahusika wa uhalifu huo, pia waangalie namna ya
kudhibiti uhalifu wakati huu ambapo wananchi wanauza mazao yao ikiwemo pamba.
Naye Diwani wa Kata ya Nyangokolwa Charles Nkenyenge amesema
kuwa katika kata yake pia kuna mwananchi amewahi kutekwa na watu wanaosafirisha
abiria ambapo walimteka na kumnyang'anya fedha pamoja na kumtishia kumuua.
Diwani wa Kata ya Mhango Martine Singibala amesema tatizo la
kutekwa wananchi limekithiri huku akilitaka Jeshi la Polisi kuongeza nguvu
kufanya ukaguzi wa magari ya abiria.
"Mwananchi wangu alitekwa na wenye magari, gari lilitoka
mjini lilielekea katani kwangu (Mhango), mwananchi akalisimamisha...baadae
likageuza safari huku wakipiga mziki mkubwa na hawakusimamishwa na maaskari,
yule mwananchi alinyang'anywa laki tatu na kutelekezwa njiani akarudi kutoa
taarifa kwa Diwani" amesema Singibala.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi
wilaya ya Bariadi Peter Ntinginya amewataka Madiwani kuwataarifu wananchi kutoa
taarifa Kituo cha Polisi pindi wanakutana na masuala ya uhalifu na Unyang'anyi.
"Wilaya yetu ina Kata 31, hivyo Polisi ni wachache lakini
tunajitahidi angalau Kila Kata kuwa na Polisi Kata mmoja, pia Kuna Kata zingine
zinakaimiwa na Polisi mmoja....wananchi wanatekwa na kunyang'anywa watoe
taarifa Kituo cha Polisi kwa hatua zaidi sababu magari hayo yamesajiliwa"
amesema Ntinginya.
No comments
Post a Comment